Kenya ‘Lionesses’ mabingwa wa raga Afrika

Muktasari:

Hii ni hatua kubwa kwa kikosi cha Kocha Kevin Mwema Wambua, kwani katika kipindi cha miaka minne imekuwa ikiburuzwa katika mchezo huo.

Nairobi. Hatimaye timu ya taifa ya wanawake ya Kenya, katika mchezo wa raga, kwa wachezaji saba Lionesses 7s wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa Afrika.

Hii ni hatua kubwa kwa kikosi cha Kocha Kevin Mwema Wambua, kwani katika kipindi cha miaka minne imekuwa ikiburuzwa katika mchezo huo.

Katika mchezo wa fainali uliopigwa jana jioni, Jijini Gaberone, Botswana, wanadada hao waliwabwaga majirani zao Uganda kwa ushindi wa 29-7. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Lionesses walikuwa kifua mbele kwa mabao 22-0 kutokana juhudi binafsi kutoka kwa Janet Akello na Michelle Omondi waliopiga 'Tries' mbili kila mmoja.

Hata hivyo, Uganda waliamka katika kipindi cha pili, wakifunga 'try' ya kwanza na pekee kupitia kwa Grace Auma, lakini Kenya walikuwa wepesi kujibu mashambulizi na kujiandikia 'try' nyingine na ya ushindi, iliyofungwa na Linet Moraa.

Kenya ilijikatia tiketi ya kutinga fainali kwa kuichakaza Madagascar 27-0 huku wapinzani wao Uganda wao wakitinga fainali kwa ushindi wa 10-5 dhidi ya Tunisia.

Safari ya kuelekea ubingwa ilianza kwa kishindo, walipotoa kichapo cha mbwa mwizi kwa Madascar (42-0) na Senegal (41-1), kabla ya kuwaburuza Zambia 43-7. Mabingwa hao walijiandikia alama 184 huki wakiweka rekodi ya kufunga 'tries' nyingi (30) na mitupio 17. Lionesses walipoteza alama 12 tu.