Harding athibitisha ushiriki KCB Karen Master 2018

Wednesday July 11 2018

 

Nairobi. Nyota wa mchezo wa Gofu nchini Afrika Kusini, Justin Harding, ni miongoni mwa wachezaji 156, kutoka mataifa 21 pamoja na chipukizi wanne wamethibitisha kushiriki michuano ya mwaka huu ya KCB Karen Masters, yatakayotimua vumbi kuanzia, Julai 19 hadi 22, katika viwanja vya Karen County Club.

Kenya itawakilishwa na maproo 32, ambao wanaifanya Afrika kuwa na zaidi ya asilimia 75 ya ushiriki katika michuano hiyo, iliyovutia mataifa mengine kote duniani. Mataifa mengine ya Afrika yanawakilishwa na maproo 20.

Kwa mujibu wa wadhamini wenza wa michuano hiyo kampuni ya simu ya Safaricom, kupitia mwakilishi wake, Steve Okeyo, michuano ya mwaka huu, yatahudhuriwa na waandaaji wa michuano mikubwa ya dunia ya Gofu, PGA Tour.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi udhamini wao kwa waandaaji wa michuano hiyo, Okeyo alisema muitikio kutoka kwa wadau wa mchezo huu, unaridhisha na kuongeza kwamba, watajitahidi kuhakikisha wanafanya michuano hiyo kuwa na mvuto wa kimataifa.

Wakiwa wadhamini wenza wa michuano hiyo, kampuni ya Safaricom ilikabidhi hundi ya shilingi milioni tano ambazo zitatumika kwa ajili ya usimamizi na uendeshaji wa mashindano, ikiwa ni pamoja na kuhahakisha usalama wa wageni kutoka mataifa mengine kama USA, Chile, Brazil, Australia na England.

“Michuano ya mwaka huu, yatakuwa na ushiriki wa timu kutoka ndani na nje ya nchi, maandalizi yanaendelea vizuri tu. Tunategemea kuwa mwaka huu, mashabiki watajitokeza kwa wingi. Kingine ni kwamba, tunategemea uwepo wa PGA Tours," alisema Okeyo.

Advertisement

Jumla ya shilingi milioni 15 zimetengwa kwa ajili ya kutoa zawadi kwa washindi ambapo mshindi ataondoka na kitita cha shilingi milioni 2.3.

Advertisement