Hakuna wa kuwazuia Gor Mahia yagawa dozi tu

Thursday August 2 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Wameshindikana. Hawakamatiki. Wanatesa tu! Hiyo ndio kauli inayofaa kuelezea fomu ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Kenya (KPL), Gor Mahia baada ya kuongeza gepu ya pointi kwenye msimamo wa KPL msimu huu hadi kufikia pointi 15.

Mabingwa hao mara 16 wa KPL, wana mechi tatu mkononi, wameonyesha kuwa wao ni moto wa kuotea mbali baada ya kuitungua Kariobangi Sharks kwa mabao 3-0, katika mechi ya KPL, iliyopigwa kwenye dimba la Moi, mjini Kisumu, wakiwapumzisha nyota wao nane.

Mabao ya Kevin Ade Omondi, Lawrence Juma na bao la kujifunga la Godfrey Shiveka, yalitosha kabisa kuwazima Sharks ambao walidhaniwa kuwa na ubavu wa kuwa timu ya kwanza kuwatoboa Kogalo kwenye ligi msimu huu.

Ushindi huo ambao ni wa nane mfululizo kwa Kogalo kwenye ligi, unakuja siku chache baada ya kuitandika Yanga SC 3-2 kwenye mechi ya marudiano ya Kombe la shirikisho huko Dar es Salaam, ni salamu kwa wapinzani na mwanzo mzuri wa kuukabili mwezi wa Agosti.

Mpaka sasa, kikosi cha Dylan Kerr, kinachokabiliwa na ratiba ngumu mwezi huu, kimeshafikisha pointi 55, pointi 15 juu ya Sofapaka inayoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi zao 40, ambapo kama  wataendelea na fomu yao ya sasa ni dhahiri kuwa hakuna wa kuzuia azma yao ya kutetea ubingwa wa KPL.

Kikosi cha Gor Mahia: Shaban Odhoji, Innocent Wafula, Godfrey Walusimbi, Haron Shakava, Charles Momanyi, Cercidy Okeyo, Boniface Omondi, Lawrence Juma, Ephrem Guikan, Bernard Ondiek, Francis Kahata.

Advertisement

Akiba: Fredrick Odhiambo, Raphael Asudi, Wesley Onguso, Joash Onyango, Wellington Ochieng, Samuel Onyango, Kevin Omondi.

Kikosi cha Kariobangi Sharks: Brian Bwire (Kipa), Bolton Omwenga, Pascal Ogweno, Godfrey Shiveka, Michael Bodo, Patillah Omotto, Sven Yidah, Harrison Mwendwa, Duke Abuya, Shaphan Oyugi, Erick Kapaito

Akiba: Gad Matthews (Kipa), Wycliffe Ochieng, Henry Juma, Ebrimma Sanneh, Francis Manoah, Sydney Lokale, Vincent Wasambo

 

Advertisement