Salha awa Miss Tanzania

Monday September 12 2011

By new

Imani Makongoro SALHA Israel (18) ameibuka malkia wa kinyang'angiro cha Miss Tanzania baada ya kuwabwaga wenzake 29 na kujinyakulia zawadi zenye thamani ya Tsh. 80 milioni kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Salha amekuwa mrembo wa kihistoria Tanzania kwa kupata zawadi zenye thamani kubwa kiasi hicho kutokana na kupata gari mpya aina ya Jeep Patriot yenye thamani ya sh 72 milioni na fedha taslimu sh8 milioni. Hii ni zawadi kubwa kabisa kwa miaka 18 ya urembo akivunja rekodi ya mwaka 2003 ya Sylvia Bahame aliyezawadiwa gari aina ya Nissan Hardbody yenye thamani ya sh 55 mil na fedha taslimu sh. 7 mil. Haikuwa rahisi kwa Salha ambaye pia ni Miss Ilala kushinda nafasi hiyo ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Dunia (Miss World) yaliyopangwa kufanyika jijini London kutokana na ushindani uliokuwa wa karibu dhidi ya warembo wengine. “Ushindani ulikuwa mkubwa sana, nashukuru kwa kupata taji hili siamini, lakini namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kupata taji hili,” alisema Salha huku mabaunsa wakimzuia kufanya mahojiano na vyombo vya habari. Tracy Sospeter aliyekuwa akiuwakilisha mkoa wa Shinyanga alishika nafasi ya pili na mrembo wa Kanda ya Ilala tena, Alexia Williams alishika nafasi ya tatu. Jennifer Kakolaki wa Ilala aliibuka wa nne huku mkoa wa Lindi kupitia Lovennes Flavian ukiibuka kuwa wa tano. Tracy alipewa kitita cha sh. 6.2milioni kwa kuwa mshindi wa pili, Alexia alipewa sh. 4 milioni kwa kuwa mshindi wa tatu. Jeniffer aliibuka na sh. 3milioni kwa kuwa mshindi wa nne huku Loveness akipewa sh.2.4milioni kwa kuwa mshindi wa tano. Warembo wengine walioingia hatua ya 15 bora na kuibuka na fedha taslimu sh.1.2milioni kila mmoja ni Mwajabu Juma (Temeke, Miss Top Model), Rose Hurbert (Kaskazini, Vipaji) na Alexia Williams (Ilala, Miss Personality). Wengine ni Tracy Mabula (Kanda ya Ziwa, Miss Photogenic), Loveness Flavian (Kanda ya Mashariki, Mrembo bora wa michezo). Waliopata zawadi ya kifuata jasho cha sh. 700,000 ni Weirungu David, Neema Mtitu (Chuo Kikuu Huria), Zerulia Manoko , Christina Mwenegoha (Kanda ya Kati) na Dalila Ghribu, Maua Kimambo (Kanda ya Kati). Wengine ni Blessing Ngowi, Glory Lory (Elimu ya Juu), Zubeda Seif (Kanda Kaskazini), Husna Maulid (Kinondoni), Atu Daniel, Leila Juma (Nyanda za Juu Kusini) , Asha Saleh (Mashariki), na Glory Samwel wa Kanda ya Ziwa. Mashindano hayo yalipambwa na burudani safi kutoka kwa wanamuziki wa Tanzania huku Sharobaro akishika nafasi ya juu kwa kukonga nyoyo za mashabiki kwa jinsi alivyotawala jukwaa. Naye John Maganga aliyemuigiza marehemu Michael Jackson aliamsha pia furaha zaidi za mashabiki. Wasanii wengine waliotumbuiza usiku huo ni Akili the Brain aliyetamba na kibao chake cha Regina, Juliana na Diamond.

Advertisement