HERSI: Kwa Yanga hii hata Mazembe tunang’oa

MABOSI wa Yanga wanakimbizana na muda ili kufanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu yao, lakini pia wakiwaza kukiborsha kikosi chao ili kurejesha heshima ndani ya Ligi Kuu Bara.

Yanga inaumaliza msimu wa tatu mfululizo mikono mitupu katika ligi hiyo, jambo ambalo ni la mara ya kwanza tangu walivyotoka kapa kwa misimu huyo kuanzia 1999-2001.

Mambo yote hayo na utekelezwaje wake upo, uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla ukaona kuna haja ya kushirikiana na mmoja wa wadhamini wao Kampuni ya GSM kutekeleza kibabe na kuwafunga mdomo wote wanaoichukulia poa klabu hiyo kongwe.

Jambo hilo lililifanya Mwanaspoti kumtafuta Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Mhandisi Hersi Said ambaye alifanya ziara fupi katika ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd inayozalisha gazeti hili na yale ya Mwananchi na The Citizen.

Hersi katika mahojiano maalumu amefichua mengi ikiwamo namna wanavyotaka Yanga iwe na uwezo wa kumsajili mchezaji yeyote hata kama anatoka TP Mazembe, moja ya klabu kubwa Afrika, huku akianika namna Kocha Luc Eymael anavyotaka majembe ya maana kikosini. Endelea naye...!

MABADILIKO YAMEANZA?

“Ndio, mchakato umeshaanza katika hatua za awali, wenzetu hawa (La liga) wameanza na hatua ya kukusanya taarifa, maswali yao mengi sasa kuja kwetu yamekuwa yanaegemea katika taarifa ambazo klabu yetu inazo kwa mfano wanataka kujua utaratibu mzima wa uongozi. Jinsi mfumo wa uongozi ulivyo, klabu inaongozwaje, kama kuna bodi, Kamati ya Utendaji, pia kama kuna bodi ya wadhamini na cheo cha juu ni Mwenyekiti au Mtendaji Mkuu au Katibu Mkuu na idara zingine zilizo chini ya Yanga zipo ngapi?” Anaeleza Hersi na kuongeza:

“Mengine walitaka kujua klabu ina uwanja kama upo ukoje? Utaratibu wa kuuza tiketi na ukusanyaji wake mapato. Lakini, bahati mbaya bodi ya ligi ndio husimamia hili sio klabu. Pia wametaka kujua mapato ya viwanjani yanapewa usimamizi wa aina gani, kwa kweli yapo mengi ambayo wameyataka na kama msisitizo wetu ni kwamba, tutawapa taarifa sahihi ili tuweze kupata tiba kwa kuvuna elimu kutoka kwa hawa wenzetu.”

BAADA YA HAPO SASA

“Hatua ya pili sasa inakuwa kuanza kuzichambua hizo taarifa tulizowapa wataangalia sasa kipi kipo nyuma wapi tunahitaji msaada na baada ya kumaliza hayo yote sasa ndio watakuja na mapendekezo kulingana na yale waliyoyabaini kupitia maelezo yetu ya awali.

“Baada ya kuwapa taarifa hizi wameshatujulisha kwamba, Juni 30 wataanza na kikao cha kwanza cha kazi ambacho kitakuwa na sura mbili wao Laliga na Sevilla na upande wa pili tutakuwa sisi na idara mbalimbali za klabu kama idara ya fedha, idara ya sheria, mawasiliano, masoko, sekretarieti na idara zingine zote.

KITAKACHOFANYWA LA LIGA

“Wanachotaka kuja kufanya lipo katika sehemu ya kwanza ya kazi, sehemu hii kuna mambo matatu yanakwenda kufanyika. Kwanza ni juu ya umiliki wa klabu, aina gani ya umiliki tunataka twende nao, sote tunafahamu kwamba asilimia 100 sasa Yanga inamilikiwa na wanachama, sasa tunaweza kusema bado tunataka klabu ibaki chini ya umiliki wa wanachama ni mfumo gani sasa tutautumia.

“Kifupi kuna umiliki wa aina tatu, ule wa asilimia 100 inamikiwa na wanachama, aina ya pili ni 100 inamilikiwa na mtu binafsi kama vile klabu ya Chelsea inavyomilikiwa na Roman Abromavich akiwa ndiye mwenye maamuzi ya kila kitu na aina ya tatu ya umiliki ni ile ya mchanganyiko sasa kati ya mtu binafsi na wanachama kwa maana ya mgawanyo wa asilimia ambapo, Yanga nadhani inaweza kwenda huko katika wanachama kumiliki asilimia 51 na mwekezaji 49.

“Yanga tutachagua katika aina hizo tatu za umiliki ipi tutataka kwenda nayo na ninavyoona kwa kanuni na sheria za nchi tutaangukia katika aina hiyo ya tatu au ya kwanza ambayo ndio zinakubalika nchini,” anasema Hersi na kuongeza;

“La pili ambalo litafanyika kwenye hii sehemu ya kwanza ya kazi ni kutengeneza sura ya uongozi, sasa hivi klabu yetu tunafahamu ipo chini mwenyekiti au tunahitaji Rais, klabu ipo chini ya katibu mkuu tutahitaji Mtendaji Mkuu na mambo mengine hivyo, lazima twende na mabadiliko. Ila kabla ya kufanya maamuzi tufahamu tofauti ni ipi kati ya nafasi tulizonazo na zile ambazo tunataka kuwa nazo? Tutaangalia pia wanapatikanaje lakini pia majukumu yao yatakuwa ni yapi, watakuwa wanawajibika kwa nani, nani atakuwa anafanya maamuzi hapo tutakuwa tumejifunza kisha kufanya maamuzi sahihi.

MABADILIKO YA KATIBA

“Hilo halina kipingamizi lazima mabadiliko ya katiba, unajua unaposema mfano labda mmeamua kubadilisha umiliki kuwa ni ule wa asilimia 49 na 51, lazima mabadiliko yatambulike ndani ya katiba, ukisema mtaamua kuwa na Rais na sio Mwenyekiti lazima katiba itambue hilo, hivyo mabadiliko mengi ambayo yatafanyika lazima yalazimishe mabadiliko ya katiba,” anasema.

“Eneo la tatu pia ambalo lina umuhimu mkubwa katika mabadiliko ni eneo la upatikanaji wa wanachama, tutafanya uamuzi wa umiliki wa klabu, tufanya mabadiliko ya uongozi na suala la upatikanaji wa wanachama hapa tunamaanisha nini, kwa mfano sasa hivi klabu ya Yanga inamtambua mwanachama wa klabu, ambaye amesajiliwa katika utaratibu wa kawaida, haimtambui mwanachama ambaye atasajiliwa kwa njia ya mtandao.

Lakini, sasa unaweza kutengeneza utaratibu wa mtu akiwa na simu yake anaweza kutumia utaratibu kujisajili na kuwa mwanachama wa Yanga ukakimbia urasimu kwamba, mtu anasumbuka anatakiwa kwenda kwenye tawi, mtafute mwenyekiti katoe kivuli cha nyaraka hizi mara karatasi hakuna.

“Ukiweka milolongo mingi kuna watu wataona kero, muda ni mchache mtu anaweza kuona huu ni utaratibu mgumu na kuona anachoka anaachaa na kiu yake ya kuwa mwanachama na klabu inapoteza pesa, mambo lazima yaende kisasa tunataka mtu ukimwambia kuna utaratibu rahisi wa kuwa mwanachama haraka anafuatilia na kujisajili.”

ELIMU KWA WANACHAMA

“Kitu ambacho tumekizingatia kwa nafasi kubwa ni eneo hilo la wanachama kupata elimu, tutatumia matawi kufikisha elimu hiyo. Hatua ya kwanza lazima watambue mkataba huu wa La Liga na Yanga ni nini wapewe elimu na kila hatua ambayo itakuwa ikipigwa katika mchakato huu itapitia huko na kisha kuletwa mapendekezo yao juu na mwisho tutakuwa na mikutano mikuu tukifika huko hakuna mwanachama, ambaye atakuwa mgeni.

DILI LA JEZI FRESHI

Akizungumzia mikataba miwili ya GSM waliyowekeza ndani ya Yanga ni kwamba hatua zimeshafanyika kwa mikataba hiyo kuongezwa baada ya klabu hiyo kuridhishwa na miaka ya kwanza ya mikataba hiyo hapa Hersi anaeleza: “Mkataba wetu wa udhamini wa magodoro mwanzo tulisaini kwa mwaka moja na hivi ninavyoongea tulishaongeza mkataba mwingine wa mwaka mmoja ulioboreshwa. Lakini, mkataba mkubwa ulikuwa ni ule wa jezi nao tumeshauongeza na hatua nzuri zaidi huu wa sasa wa jezi pia utahusisha vifaa mbalimbali kama skafu na vitu vingine mbalimbali ambavyo watu wengi walikuwa wanaviulizia.”

MKWANJA WA MAANA YANGA

“Niwaambie hapa watu wa Mwanaspoti mkataba wetu wa jezi kwa Yanga umeifanya Yanga kuwa klabu iliyoingiza fedha nyingi msimu huu ambao unaelekea ukingoni kuliko nyingine. Tena kuna klabu kubwa tunaambiwa imepata kama sh 100 milioni lakini Yanga wamevuna fedha nyingi, sitaki kueleza wazi kila kitu lakini kwa jinsi makubaliano ambayo tuliingia na Yanga kwa pesa ambayo waalikuwa wanapata kwa kila jezi hakuna klabu itakuwa imeingiza fedha kuwazidi wao.

JEZI MPYA HATARI

“Baada ya kuona jinsi watu walivyoipokea jezi ya kwanza safari hii tumeona tuiboreshe zaidi, na tayari tulishafanya ubunifu wa jezi na kuishirikisha klabu na imekubalika na wakati tunaanza mtakumbuka kulikuwa na changamoto mbalimbali za ujio wa jezi. Lakini, safari hii mambo yatakuwa tofauti tumeanza mapema na jezi ya safari hii itakuwa na heshima kubwa zaidi.

USAJILI UPO HIVI

Kuhusu usajili tuko makini na eneo hilo na kazi inaendelea kwa umakini, kuna wachezaji ambao, tumeshamalizana nao hao ni wapya wako kama watano wawili wa ndani ambao ni beki na winga mmoja nisingependa niwataje. Wachezaji wa kigeni tuna orodha ya watano na ikumbukwe kwamba, kwa sasa tuna wachezaji tisa wa kigeni katika hao tutaachana nao wanne au watano kisha tutaingiza wapya watano.

“Hao wapya sasa tayari watatu ni kama tumeshamalizana nao mambo mengi yameshakamilika kilichobaki sasa kuna wawili ambao, mazungumzo yapo hatua za mwisho kabisa tukisubiri nyaraa muhimu za malipo. Tunasubiri mipaka ya baadhi ya nchi ifunguliwe tu, wachezaji waanze kutua nchini. Nisisitize kwamba, Yanga hata ikitaka mchezaji TP Mazembe au AS Vitta tutamleta, sisi sio kama klabu zingine watu wasishangae kuna wachezaji watatoka upande wa pili na kuja Jangwani.

PANGA YANGA?

“Kama nilivyosema kwa wachezaji wa kigeni tutapunguza wanne na kuingiza watano kutokana na bado tuna nafasi moja ya wazi katika zile 10 za kikanuni. Kwa hapa ndani kuna wachezaji kama tisa hivi ambao wanamaliza mikataba yao kati ya hao tunatarajia kuwaongezea mikataba wachezaji wanne tu au watano wengine tutaangalia kuwatoa kwa mkopo au kuachana nao.

MBELGIJI ATAKA 26 TU

“Tumekuwa tunafanya kazi hii ya kuboresha timu tukishirikiana kwa karibu na kocha Luc Eymael na hakuna mchezaji tunafanya naye mazungumzo bila kumshirikisha na kwa msimu ujao anataka awe na kikosi chenye wachezaji 26 pekee na sio zaidi ya hapo, lakini msisitizo anaoutaka ni kuwa na kikosi chenye ushindani na ubora mkubwa.

ISHU YA MWAMNYETO

“Ndio tunamtaka beki Bakar Mwamnyeto na usajili huu una hatua mbili ya kwanza ni kuzungumza na klabu yake kutokana na kuwa bado na mkataba wa mwaka mmoja na nusu. Hatua iliyopo ni kwamba, tayari tumekubaliana na Coastal Union, karibu kila kitu na wakatupa nafasi ya hatua ya pili sasa kuongea na mchezaji nako kila kitu kipo sawa tunachosubiri kuna msimamizi wake, ambaye anaishi Italia ili naye awepo kwenye hatua za mwisho na kumalizana kila kitu.

UTATA WA MORRISON

“Kuhusu mchezaji Bernard Morrison nafikiri klabu imemaliza kila kitu sitaweza kutoka nje ya hapo. Morrison hata nikisimama leo na nikaambiwa nishike vitabu vya dini nitasema ni mchezaji wa Yanga kwa kuwa sasa yupo ndani ya mkataba wa miezi sita ya awali na tulipovutiwa na kipaji chake tukakubaliana kuongeza mkataba. Amesaini mkataba na kwa macho yangu nilishughudia mbele ya mwanasheria sioni utata wowote.

Kuhusu kwa nini Morrison anadai hajasaini mkataba? Hersi anasema; “Kitu ambacho nakiona ni tamaa ya mchezaji mwenyewe, aliwahi kunifuata akiniambia alipata ofa katika klabu nyingine akiona ni nzuri kuliko yetu na anaomba mkataba uvunjwe na sikuwa na jibu lingine zaidi ya kumwambia hiyo ofa inakujaje wakati anajua yupo ndani ya mkataba na Yanga?

“Morrison anatakiwa kufanya kazi yake kama kuna klabu inamtaka utaratibu unajulikana watambue kwamba, huyu ni mchezaji halali wa Yanga na klabu ina makao yake makuu na uongozi walete ofa kwa klabu.

“Kuna mambo ya hovyo yanafanyika kwa klabu moja kumfuata Morrison na kuzungumza naye hili ni kosa kubwa na ni hatari... hatutakuwa na urafiki na mambo ya namna hii tutachukua hatua kali na niseme zipo hatua tumeshaanza kuzichukua kwa wale wanaofanya hivi, watu wafuate utaratibu hatutakuja kukaa mezani na kwa makosa ya namna hii.

TSHISHIMBI BADO

Hersi akimalizia kufafanua kuhusu usajili, pia alielezea hatua za Papy Tshishimbi kuongeza mkataba akisema: Tshishimbi ni kweli bado hajasaini mkataba ni mchezaji wetu, tulimuita na kuzungumza naye na tukakubaliana yale ambayo tunataka kuyafanya, lakini wakati wowote kutoka sasa mtasikia na kuona amesaini mkataba.