Kwa Class! Mbona huyo Msauzi anakaa mapema tu

Friday November 24 2017

 

By IMANI MAKONGORO

SAA chache tu kabla ya pambano lao la ubingwa wa dunia, mabondia Koo’s Sibiya wa Afrika Kusini na Mtanzania Ibrahimu Class, wametambiana huku kila mmoja akijinasibu kuondoka na taji hilo.

Pambano hilo la ubingwa wa dunia unaotambuliwa na Chama cha GBC, litapigwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na litakuwa la raundi 12.

Tayari majaji na mwamuzi wa pambano hilo kutoka Ujerumani, Kenya na Uganda wamekwisha wasili Dar es Salaam na leo Ijumaa watashuhudia upimaji uzito na afya kwa mabondia hao utakaoanza saa 4 asubuhi pale Uwanja wa Taifa.

Koo’s na Class jana Alhamisi walikutana kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam ikiwa ni saa chache baada ya Koo’s kuwasili nchini ambapo kila mmoja alijinasibu kuondoka na taji hilo la dunia kesho.

“Nimekuja Tanzania kwa kazi moja tu ya kuchukua ubingwa na kurudi nao Afrika Kusini, najua pambano litakuwa gumu, lakini nimekuja kushinda na si vinginevyo,” alisema Koo’s.

Class alijibu kwa kusema mpinzani wake asitarajie mteremko Jumamosi na kusisitiza kwamba ‘atamsurubu’ raundi za mapema tu kwani uwezo huo anao.

“Nimejiandaa vizuri, niko fiti kweli kweli, yaani kama mpinzani wangu atamaliza raundi zote 12 atakuwa amefanya kazi, sitowaangusha Watanzania na niwaombe tu nao wajitokeza wanisapoti,” alisema Class.

Promota wa pambano hilo, Joe Enes, alisema maandalizi yote yamekamilika na pambano litaanza saa 8 mchana likitanguliwa na mapambano kadhaa ya utangulizi.