Kikapu Arusha washindwa kushiriki Taifa Cup

Monday November 20 2017

 

By Yohana Challe

Arusha: Chama cha mpira wa kikapu Mkoa wa Arusha (ARBA) kimeshindwa kupeleka timu hata moja katika mashindano ya Taifa ya kikapu yaliyoanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki Jijini Dar Es Salaam.

Mjumbe wa Mashindano wa ARBA, Barrick Kilimba alisema wameshindwa kushiriki michuano hiyo kutokana na kutofanyika mashindano ya Kanda ya kaskazini mwezi uliopita Mkoani Tanga kwa sababu ya mvua iliyokua inanyesha mfululizo katika siku ambazo mashindano yalipaswa kufanyika.

 “Mashindano ya Kanda yalikuwa yanashirikisha mikoa minne Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga ndio ilikuwa inatoa fulsa kwa timu mbili za juu kwenda kwenye michuano ya Taifa itakayotoa Bingwa wa Taifa,” alisema Kilimba.

Aliongeza kuwa kutokana na kushindwa kufanyika mashindano hayo bado shirikisho la Kikapu Taifa (TBF) ilichelewa kutoa taarifa juu ya mashindano hayo ambayo ARBA walipewa taarifa siku mbili kabla ya mashindano ya Taifa kufanyika na ndipo Mkoa wa Tanga na Manyara zikapewa fulsa ya kuiwakilisha kanda kwenye mashindano.

 Jumla ya Timu 20 zinashiriki michuano hiyo huku kwa upande wa kanda ya kaskazini ikiwakilishwa na timu ya Manyara Kings huku Tanga wakituma Timu mbili Queens ya wanawake na Bandari ya Wanaume.

 Kwa Mujibu wa TBF timu 12 zitakuwa za wanaume na nyingine za wanawake zinashiriki michuano kati ya hizo ni Don Bosco (Dodoma) , kutoka jijini Dar es Salaam kuna Savio, JKT, DB Lioness, Vijana Queens, Risasi Wanaume na wanawake (Shinyanga) na Mwanza Profile.