Hizo ngumi za Class lazima ukae

Monday November 27 2017

 

By IMANI MAKONGORO

KUNA watu wanapiga ngumi nyie, usiombe kukutana nao. Mmoja wao ni Ibrahim Class ambaye juzi Jumamosi alitetea taji lake la dunia linalotambuliwa na GBC.

Class alimtwanga Msauzi Koos Sibiya makonde ya maana mpaka damu zikaanza kuruzika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Ilikuwa ni balaa tupu. Waswahili wanasema usithubutu kukutwa na makonde ya Class.

Mwenyewe anasema lile nyomi la mashabiki pale uwanja wa Uhuru ambalo karibu wote lilikuwa likimshangilia ndiyo siri ya kurusha ngumi zile za kuua mtu.

Class anakwambia ilikuwa lazima ashinde licha ya mpinzani wake, Koos Sibiya wa Afrika Kusini kuwa na nguvu za ajabu na kumpa wakati mgumu, lakini yeye ilikuwa ni lazima ashinde kwa namna yoyote ile kabla ya kutangazwa bingwa kwa pointi za majaji 3-0 wa uzani wa super feather.

“Yule Msauzi ni bondia mwenye nguvu mno, kwa kweli kama sio maandalizi niliyoyafanya, pengine yangekuwa mengine leo. Nilidadisi alifanya maandalizi ya pambano hili kwa muda gani akaniambia miezi sita, mimi nilijiandaa kwa miezi mitatu.

“Pamoja na yote, nashukuru kuona nimeshinda na kutetea ubingwa wangu, kiukweli nilihamasika sana kuona karibu mashabiki wote uwanjani wako upande wangu, hamasa yao imenipa ubingwa huu kwa mara nyingine,” alisema Class.

Pambano lilivyokuwa

Koos ndiye alianza kupanda ulingoni saa 3:10 usiku akisindikizwa na wasaidizi wake wawili kabla ya Class kupanda dakika mbili baadae akiwa katikati ya mashabiki waliokuwa wamemfunika kwa bendera ya Taifa.

Refarii, Arno Pokrandie wa Ujerumani alianzisha pambano saa 3:15 Usiku,  lakini Msauzi ndiye alikuwa wa kwanza kuanzisha mashambulizi kwa kumpiga konde Class kwa staili ya kudokoa.

Msauzi huyo alionekana kucheza kana kwamba anamsoma Class na hadi raundi ya kwanza inamalizika uzani ulikuwa sawa.

Raundi ya pili Class alianza kwa kumsoma mpinzani wake ambaye aliendelea kujiamini na kucheza masumbwi ya nguvu kabla ya Class kuwaamsha vitini mashabiki wa Tanzania baada ya kumtandika makonde ya nguvu mpinzani wake raundi ya tatu.

Raundi ya nne mabondia wote walicheza kwa kuviziana huku raundi ya tano, Class akimpeleka Msauzi chini lakini refarii akakataa kuwa sio ngumi ya pointi. Raundi ya sita Msauzi huyo aliianza kwa mashambulizi ya nguvu hivyo kusababisha ukimya wa muda kwa mashabiki uwanjani hapo hadi raundi ya nane huku raundi ya saba nusura Class naye aende chini.

Kuanzia raundi ya tisa, Class alianza kubadili upepo na kumshambulia kwa nguvu mpinzani wake ambaye hadi anamaliza raundi zote 12 alikuwa akivuja damu kutokana na konde ambalo lilimpata puani.

“Halikuwa pambano jepesi, Class kaonyesha Tanzania tunaweza kwani mpinzani wake hakuwa legelege kabisa, lilikuwa pambano zuri mno na la kusisimua. Nimpongeze tu Class kwa kulibakisha taji hili nyumbani,” alisema Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa mgeni rasmi juzi

Mapambano ya utangulizi

Katika hali ya kushangaza, mabondia waliozichapa pambano la utangulizi kumsindikiza Class na Koos walianzisha tafrani baada ya kupanda ulingoni kudai malipo yao dakika chache kabla ya kuanza pambano la Class.

Mabondia hao waligoma kushuka ulingoni kupisha pambano hilo la dunia kwa kile walichodai hadi wapewe chao, lakini Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja alizungumza nao na kuwaahidi kulipwa fedha zao haraka iwezekanavyo, ndipo wakaridhia kushuka kupisha pambano la Class kuendelea.

Tamba apigwa

Pambano kali la utangulizi lilikuwa kati ya Ibrahim Tamba na Ibrahim Maokola ambapo bingwa alitakiwa kuzichapa kuwania mkanda wa GBC, hata hivyo Tamba alipigwa kwa pointi.

Pambano jingine, Adam Yahaya na Shafii Ramadhan walitoka sare huku Feliche Mashauri akimpiga Happy Daudi kwa pointi za majaji 3-0 na Lulu Kayage akimtambia Mwanne Haji kwa pointi za majaji 2-1.