JICHO LA MWEWE: hii ndio Kazi nzito inayomkabili Haruna kwa Clatous Chama

Monday December 10 2018

 

By Edo Kumwembe

TULIWAHI kuwa na mchezaji anayeitwa Athuman Juma Chama ‘Jogoo’. Mwingine Rashid Idd Chama. Hawa walipewa majina haya kutokana na beki wa pembeni Mzambia aliyeitwa, Dick Chama.

Baadaye kizazi kingine kikawa na mchezaji anaitwa Chama Jumapili. Wote walikuwa Watanzania. Sasa kwa mara ya kwanza tuna mchezaji anayeitwa Chama anatoka nje ya nchini. Clatous Chama. Anatokea Zambia.

Nimemtupia jicho mara kadhaa nimegundua ana vitu vya ziada. Tuna wachezaji wengi wa kigeni wanaocheza nchini. Wachache wanabakia kuwa mfano kwa waliopo. Vilevile wanabakia kuwa mfano kwa vijana wanaotaka kujifunza mpira.

Huyu Chama wa Simba ni fundi. Kila anapocheza mpira huwa naiwaza nafasi ya Haruna Niyonzima. Miezi 18 iliyopita kulikuwa na vurugu za Haruna Niyonzima kwenda Simba, Ibrahim Ajib kwenda Yanga. Wote walikuwa wamemaliza mikataba yao.

Haruna alichukua pesa nyingi kwa watu wa Simba kwa ajili ya kuhakikisha hasaini Yanga. Simba iliamini ilikuwa imempata mchezaji wake ambaye kwa muda mrefu alikuwa anavaa jezi za Yanga lakini ilikuwa wanamuona amekaa Kisimbasimba zaidi. Kama wakati ule ilivyokuwa inamuona Thaban Kamusoko.

Kuanzia hapo Simba haijamfahidi Niyonzima na sidhani kama itamfahidi tena. Iko wapi nafasi yake? Siioni sana. Amerudi vema lakini nafasi yake ya kuwa Niyonzima yule ambaye tuyelimzoea itakuwa ngumu. Itabidi afanye kazi mbili.

Huyu Chama ninavyomuona ana uwezo wa kucheza aina ya mchezo wa Haruna, halafu vilevile akawa na madhara zaidi. Watanzania wanapenda mpira wa mbwembwe na manjonjo. Niyonzima aliiwezesha mioyo ya Watanzania kwa staili hiyo. Lakini Chama anaweza kufanya hivyo na ataenda mbali zaidi kwa kuleta madhara.

Anapiga pasi nyingi za mwisho. Anafunga. Mabao mawili aliyofunga dhidi ya Mbabane Swallows ugenini yalikuwa muhimu zaidi kwa Simba. Bao lake moja tu la kwanza lilishatosha kuivusha Simba kwenda katika hatua nyingine. Kabla ya hapo alishafunga bao la nne katika pambano la kwanza.

Kwa kocha ambaye anaielewa vema kazi yake itakuwa vigumu kuwapanga Niyonzima na Chama pamoja. Jaribu kufikiri, kama Chama na Hassan Dilunga hawawezi kucheza kwa pamoja, vipi kwa Niyonzima? Wote ni wachezaji wa aina moja. Wachezeshaji. Playmakers. Wanacheza huru zaidi kutoka kuhamisha mpira eneo la nyuma, au katikati kwenda mbele.

Kocha hawezi kuwapanga wawe huru. Ndio maana licha ya ubora wake, lakini Dilunga anakaa nje mbele ya Chama kwa sababu kazi yao uwanjani ni moja. Niyonzima akiitaka nafasi yake irudi inabidi afanye kazi mbili anazofanya Chama. Kutengeneza nafasi kwa wenzake na kufunga.

Kwa ufahamu wangu, Chama ni mchezaji anayependa kusonga mbele zaidi (direct player), wakati Niyonzima huwa anakwenda pembeni na kuganda zaidi (static). Ili uwe na madhara inabidi uwachanganye mabeki kwa kwenda mbele mara nyingi na kutafuta kitu.

Nini kinafuata kwa Niyonzima? Maisha ya soka yanakwenda kasi sana. Ukipata nafasi yako katika timu kubwa inabidi uichukue na kuitumia kwa haraka. Sidhani kama kinachotokea sasa kwa Niyonzima alikitazamia. Sidhani. Nadhani hakujua kama Simba itamleta mchezaji ambaye atafanana naye kwa kila kitu halafu atakuwa bora zaidi.

Katika msimu wake wa kwanza alipaswa kuikamata Simba na kuiweka mfukoni mapema. Hata hivyo, kuna mambo mawili yalitokea. Kwanza alipata bahati mbaya ya majeraha, lakini pia akapotea klabuni. Wakati timu ikiwa Istanbul, Simba ilikuwa haijui Niyonzima alikuwa wapi. Mambo haya yalipaswa kutokea wakati tayari ameiweka Simba mkononi.

Huu ndio ujanja wa Ajib. Ana matatizo yake na klabu lakini anafunga kama kawaida. Anapika mabao. Akileta uvivu anauleta akiwa anajivunia kwa kile ambacho amekifanya katika timu mpaka sasa na sio kujivunia kile ambacho aliwahi kukifanya Simba.

Haya yote yanatokea wakati Niyonzima akiwa chaguo la tatu katika eneo la kiungo mchezeshaji. Baada ya Chama anakuja Dilunga kisha Haruna. Wakati mwingine kocha wa Simba anatumia ujanja wa kumsogeza mbele Chama na kumleta Dilunga nyuma. Bado haiondoi ukweli Simba inapotimia Chama inabidi arudi nyuma kidogo huku Meddy Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi wakianza.

Kama Simba itacheza na wapinzani wagumu na kuamua kujaza wachezaji wengi wa kiungo bado siioni sana nafasi ya Niyonzima katika mfumo huo. Kama unahitaji viungo wengi na ukabaji zaidi unaweza kuwapanga Jonas Mkude, James Kotei hata na Dilunga kwa pamoja halafu bado Chama akacheza kwa juu. Nataka nione jinsi Niyonzima kama atamudu mtihani wake wa kwanza mkubwa katika soka. Tangu akiwa APR, Yanga na Timu ya Taifa ya Rwanda sijawahi kuona akiwa na changamoto ya namna hii.

Huu ndio wakati wa Niyonzima kuonyesha maana halisi ya kuwa mwanasoka bora na wa kulipwa.

Advertisement