Zlatko aliharibu hapa tu

SIKU 35 tu zimemtosha kuishi Bongo. Kocha Zlatko Krmpotic tayari ameshaondoka nchini akirudi kwao Yugoslavia baada ya juzi kutimuliwa na mabosi wa klabu hiyo kama ambavyo Mwanaspoti lilikupa taarifa ya uhakika.

Wengi waliona kama ni uamuzi wa kushangaza lakini kwa hali ya mambo na maisha ya kocha huyo kuondolewa lilikuwa ni suala la muda tu na katika mchezo dhidi ya Coastal Union licha ya kushinda kwa mabao 3-0 ilikuwa hata kama angeshinda 30-0 angefutwa kazi baada ya uamuzi kuwa tayari ulishafanyika.

Hebu sasa tuangalie yale mambo sita ambayo yalichangia kwa kiasi kikubwa kocha huyo kupoteza ajira yake hiyo akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi tano pekee za Ligi Kuu na tatu za kirafiki huku akishinda saba na kutoa sare ya bao 1-1 na Tanzania Prisons.

Mbinu zake

Mpira wa Krmpotic ulimponza Yanga haikuwa tishio sana wakati akiiongoza ndio alitaka mpira ambao utampa matokeo lakini muda mwingi Yanga haikuvutia katika macho ya wengi.

Hatua mbaya zaidi ni pale ambapo alikuwa akipenda kutumia viungo watatu wa ukabaji kwa wakati mmoja huku wakitumia mipira mirefu zaidi halikuwafurahisha mashabiki, wachezaji na hata viongozi wake na kuona sio mtu muafaka kwao.

Hataki ushauri

Ndani ya wasaidizi wake inaelezwa Krmpotic hakuwa anataka kupokea ushauri hakuna ambacho alitaka kuwasikiliza wasaidizi wake lakini pia inaelezwa kwamba kocha wa viungo, Reidoh Bardien na daktari wa viungo Fareed Caseem ni chanzo cha kuondoka katika klabu hiyo wakiomba kwenda kupumzika.

Kutokana na hali hiyo wasaidizi wake waliamua kumuangalia afanye uamuzi mwenyewe huku wakiumia kuona mambo hayaendi sawa na kuyawasilisha hayo kwa viongozi wa juu baada ya kuitwa katika kikao wiki iliyopita.

Kugomea kikao na mabosi

Wakati Yanga ikimaliza mchezo wa ushindi wa pili kule Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar inaelezwa Krmpotic alitaka kugomea kikao na viongozi wa klabu hiyo akisema anataka kwenda kufanya kazi zake chumbani hatua hiyo mabosi wake waliona kama ni dharau kwake kisha wakamuwekea kinyongo ndani yake na kumshtaki kocha huyo kwa wadhamini wao.

Lugha chafu kwa wachezaji

Yanga ikiwa Bukoba ikitaka kucheza na Kagera Sugar inaelezwa alimtolea lugha chafu winga, Faridi Mussa hatua ambayo iliwakera mpaka wachezaji wenzake lakini hayo ndio yalikuwa maisha yake kwa kupenda kuwa mkali lakini pia kutokuwa na lugha nzuri kwa wasaidizi wake na wachezaji wake.

Ratiba ya mazoezi yake

Ugumu mwingine wa maisha ya Krmpotic ulikuwa katika ratioba yake ya mazoezi wachezaji walimshtakia kuwa hata kama hawapendi mazoezi magumu lakini sio ya Krmpotic rekodi yake kubwa ni pale Jamhuri ambapo aliiongoza timu hiyo kufanya mazoezi kwa dakika 35 pekee na mabosi wake walipotaka kuwahi mazoezi wakakuta timu imeshamaliza na wapo ndani ya basi wanarudi kambini.

Wachezaji kuamua kujiongeza waliomba mbwa wa ulinzi kambini kwao kule Kigamboni wawahi kufungiwa ili wafanye mazoezi asubuhi sana wakihofia kuzomewa wakiwa uwanjani kwa kutokuwa fiti.

Rekodi yake ili muhukumu

Krmpotic hana rekodi kubwa ya mafanikio ukiacha ile ya Mazembe na Zesco kidogo lakini hulka yake ya kutokaa na kutimuliwa kwa muda mfupi pia iliwashawishi mabosi wa Yanga na kuona hafai.

Yanga alidumu kwa siku 35 akiwa ndio sehemu aliyokaa kwa muda mfupi zaidi lakini pale Polokwane City ya Afrika Kusini alidumu kwa siku 113,alifanya kazi pia APR ya Rwanda akakaa siku 159, Botswana alifanya kazi klabu ya Jwaneng Galaxy nako akaa siku 189 na kumalizia Zesco ya Zambia alikodumu kwa siku 165.

Tayari mabosi wa Yanga wameanza mchakato wa kupata kocha mpya huku, Juma Mwambusi na Said Maulid wataendelea kulisukuma gurudumu hadi pale mambo yatakaponyoka na kupata kocha mpya.