Zlatan kawa mtamu kinoma anatupia tu La Galaxy

Muktasari:

Mshambuliaji Ibrahimovic amekuwa na msimu mzuri katika Ligi Kuu Marekani baada ya kufunga bao na kutengeneza jingine katika ushindi ulioipeleka Los Angeles Galaxy katika hatua ya mtoano.

Minnesota, Marekani. Mshambuliaji nyota na nahodha wa zamani wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic amefunga bao na kutengeneza jingine katika ushindi wa Los Angeles Galaxy wa mabao 3-1 dhidi ya Minnesota na kuipeleka timu yake hatua ya mtoano.

Zlatan alifunga bao lake la 22 msimu huu kwa kichwa akiunganisha krosi ya Rolf Feltscher dakika ya 30 kabla ya kupika la tatu lililofungwa na Romain Alessandrini dakika ya 53 wakati Ola Kamara alifunga bao la pili dakika ya 50 baada ya kupewa pasi na Ashley Cole.

Ushindi huo umeifanya LA Galaxy kujikatia tiketi ya kucheza mechi ya mtoano ambapo itakipiga na Houston na mshindi kujikatia tiketi ya kucheza hatua inayoafuata ya nusu fainali ya Ligi Kuu Marekani.

Pamoja na kupoteza mchezo huo, lakini Minnesota iliyokuwa ikicheza mechi yake wa mwisho kwenye Uwanja wa TCF Bank, kabla ya kuhamia uwanja mpya msimu ujao, ilivunja rekodi ya mapato baada ya mashabiki 52,242 kuushuhudia mchezo huo.