Zitto, Makamba na Bashe wazungumzia kutekwa kwa Mo Dewji

Thursday October 11 2018

 

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Wabunge Zitto Kabwe, January Makamba na Hussein Bashe wamezungumzia tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji.

Kupitia katika kurasa za mitandao yao ya kijamii wabunge hao wamezungumzia tulio hilo, kueleza kuwa polisi watatoa taarifa kamili.

Makamba ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ameandika, “ nimezungumza na baba yake Mohammed Dewji. Habari za kutekwa kwa rafiki yetu Mo ni za kweli.”

“Nimetikiswa sana. Naamini polisi watatoa taarifa kamili. Mohammed ana familia na watoto wadogo.”

 Mbunge huyo wa Bumbuli amemalizia ujumbe wake kwa kusema, “Tumuombee yeye na familia yake. Tusaidie kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake.”

Kwa upande wake Zitto (Kigoma Mjini) amesema, “Nimeshtushwa na kuumizwa na habari za kutekwa kwa ndugu yetu Dewji leo alfajiri akiwa anakwenda mazoezini hapa Dar es Salaam.”

“Kila mmoja wetu mwenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kumwokoa asaidiane na vyombo vyetu vya dola. Mola atamsaidia MO na familia yake katika mtihani huu.”

Bashe (Nzega Mjini) amesema, “Inasikitisha na kushtua tukio hili la Dewji  kutekwa. Aina hii ya uhalifu inaota mizizi ana familia ana watoto ana ndugu tuendelee kumuombea kwa Allah na  kila mmoja wetu kutoa taarifa yoyote atakayopata ambayo itasaidia kumpata akiwa salama Allah amlinde.”

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema polisi wanafuatilia taarifa za madai ya kutekwa kwa mfanyabiashara huyo.

Akizungumza na MCL Digital leo Alhamisi asubuhi Mambosasa amesema baada ya kupata taarifa za tukio hilo wanafuatilia kujua ukweli wake.

Dewji ni mwekezaji wa klabu ya Simba akiwa na hisa 49 na amekuwa akiingia katika chati ya juu ya jarida la Forbes kama miongoni mwa matajiri vijana Afrika.

 

 

Advertisement