Zidane anasepa na kijiji

Muktasari:

  • Zidane aliondoka Madrid huku akiacha mafanikio makubwa ikiwamo kuweka rekodi ya kipekee ya kutwaa mataji matatu mfululizo kama kocha. Kwa nini Perez asimrudishe na chama linayumba.

MADRID,HISPANIA.KUNA mwenye swali? Hakuna haja ya kuongea saaana kuhusu Zinedine Zidane ‘Zizou’. Ndo’ hivyo, kasharudi nyumbani Real Madrid kwa mara nyingine.

Pale Santiago Bernabeu kwa sasa mashabiki watakuwa wanacheka tu baada ya Rais wa klabu hiyo Florentino Perez kuwarudishia jembe lao.

Zidane aliondoka Madrid huku akiacha mafanikio makubwa ikiwamo kuweka rekodi ya kipekee ya kutwaa mataji matatu mfululizo kama kocha. Kwa nini Perez asimrudishe na chama linayumba.

Ni miezi 10 tu imepita tangu asepe lakini sasa anarudi na wala hajali chama likoje anachojua anaenda kufanya kazi yake tu, kushinda.

Madrid kwa sasa iko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa La Liga (pointi 51) nyuma ya vinara Barcelona (63) na Atletico Madrid inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 56.

Hata hivyo, inavyoonekana Zidane hawezi akarudi tu hivi hivi na kwa taarifa yako tu, mkononi anayo orodha yake ya mastaa wa nguvu anaowataka na kama akiwapata, mtapisha njia wenyewe.

Eder Militao

Kuna uwezekano mkubwa Zidane akamnasa Eder Militao kutoka FC Porto dirisha la usajili linalokuja. Tayari Rais wa Real Madrid, Florentino Perez ameahidi kumwaga Pauni 300 milioni za usajili msimu unaokuja na Militao ni mmoja kati ya matamanio ya Zidane.

Ni kiungo mkabaji wa ukweli na ataisaidia Real wana eneo la nyuma pamoja na Sergio Ramos na Raphael Varane ambao wanaonekana kuyumba siku za karibuni.

Matthijs De Ligt

Huenda moyo wake upo Barcelona na timu hiyo ipo katika harakati za kumsajili, lakini nani ambaye hapendi pesa. Zidane amekuja na staili yake ya kutaka wachezaji wanaofanya vizuri kupewa bonasi ya juu, kizuri kinda huyo wa Ajax ni mhangaikaji uwanjani, chini ya Zizou anaweza kupata bonasi za kutosha tu. Kabla hajaondoka Real, Zizou aliwahi kumwita mchezaji huyo ajiunge na timu yake lakini mipango haikutimia.

Luka Jovic

Zidane anamfurahia Karim Benzema lakini anataka mtu wa kumsaidia. Luka Jovic wa Eintracht Frankfurt ni mtu sahihi katika hilo. Anataka amkuze na kuchukua nafasi ya Benzema baadaye. Lakini Barcelona pia inamtaka straika huyo ambaye amefunga mabao 15 katika mechi 22.

Neymar

Rais wa Real, Florentino Perez akilala anamuota Neymar wa PSG, ni rahisi kumshawishi Zidane amsajili wakati huu akitaka mchezaji mwenye kiwango cha dunia kama Neymar.

Kylian Mbappe

Zidane amekuwa akimuota Kylian Mbappe wa PSG kwa siku nyingi. Alianza kumsaka tangu 2017 akiwa Monaco, lakini PSG wakaibuka na kumnyakua kwa kitita cha maana. Huenda PSG wakawa wagumu kumwachia nyota huyo mwenye mabao 24 katika Ligi Kuu Ufaransa lakini pesa ni stori nyingine kabisa.