Zidane amvuta Mane Real Madrid

Muktasari:

Zidane ameanza kuisuka upya Real Madrid baada ya kutia saini mkataba mpya unaomalizika mwaka 2022.

Madrid,Hispania. Real Madrid imemgeukia mshambuliaji wa Liverpool Sadio Mane baada ya Zinedine Zidane kurejea Santiago Bernabeu.

Mshambuliaji huyo anatakiwa na Zidane, baada ya kuonyesha kiwango bora msimu huu akifunga jumla ya mabao 17.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Senegal, amekuwa kinara katika kikosi cha Liverpool akiwa ndiye mfungaji bora.

Zidane ameanza kuisuka upya Real Madrid baada ya kutia saini mkataba mpya unaomalizika mwaka 2022.

Hata hivyo, kocha huyo anatakiwa kufanya kazi ya ziada kupata saini ya Mane kwa kuwa ndiye mhimili wa Liverpool katika safu ya ushambuliaji.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ufaransa, Zidane amemuweka Mane katika orodha ya nyota anaowataka katika usajili wa majira ya kiangazi.

Mane mwenye miaka 26, anashika nafasi ya pili kwa ufungaji nyuma ya Sergio ‘Kun’ Aguero katika mashindano ya Ligi Kuu England.

Novemba, mwaka jana Liverpool ilimuongeza Mane mkataba ambao unamalizika 2023.

Pia Zidane anataka kutekeleza azma ya kumsajili kiungo wa pembeni wa Chelsea Edin Hazard ambaye amekuwa akimtaka muda mrefu.