Zidane alipoingia anga za Mourinho, Van Gaal

Thursday March 14 2019

 

MADRID, HISPANIA . ZINEDINE Zidane amekubali kurudi kuwa kocha Real Madrid, ikiwa ni miezi kama tisa hivi imepita tangu alipoachana na timu hiyo baada ya kuwapa mataji matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Jambo hilo linamfanya Zidane kuingia kwenye orodha ya makocha ambao walirejea kwenye klabu zao za zamani kuendelea na kazi baada ya kuachana nao awali.

Jupp Heynckes –Bayern Munich

Kocha, Heynckes alibeba mataji manne ya Bundesliga, wakati alipokuwa kocha wa Bayern Munich. Taji lake la kwanza alibeba mwaka 1989 na mengine aliyapata kwenye kipindi chake cha karibuni. Kocha huyo alianza kuinoa Bayern 1987 hadi 1991, akarudi 2009 akaondoka, akarudi tena 2011 hadi 2013 akaondoka kabla ya kurudi 2017 hadi 2018. Kwa maana hiyo, kocha huyo ameinoa Bayern katika awamu nne tofauti, mara yake ya mwisho kurudi ilikuwa 2017 wakati timu ilipomfuta kazi Carlo Ancelotti.

Kenny Dalglish –Liverpool

King Kenny alikuja kuwa kocha wa Liverpool kwa awamu ya pili mwaka 2011, ikiwa ni miongo miwili baada ya kujiuzulu kuinoa timu hiyo kufuatia lile tukio la Hillsborough. Dalglish alianza kuinoa Liverpool 1985 na kukaa hapo hadi 1991 kabla ya kuondoka na kisha kurudi tena kuinoa timu hiyo ya Anfield mwaka 2011, akidumu kwa mwaka mmoja na kisha kuondoka tena. Awamu yake ya kwanza kwenye kikosi hicho ilikuwa ya mataji, lakini aliporudi kwa mara ya pili aliishia tu kubeba taji la Kombe la Ligi, licha ya kwamba kwenye msimu huo wa 2011 -12, timu ilimaliza ligi kwenye nafasi ya nane katika msimamo.

Advertisement

Fabio Capello –Real Madrid

Mtaliano, Fabio Capello amewahi kuinoa Real Madrid katika awamu mbili tofauti. Awamu zake zote mbili zimekuwa za mwaka mmoja mmoja tu, kwanza ilikuwa 1996-1997 na pili ilikuwa 2006-2007. Kwenye awamu yake ya kwanza alishinda taji katika msimu wake wa kwanza na kuwasajili mastaa matata kabisa kama Clarence Seedorf na Roberto Carlos, lakini akaja kufukuzwa. Miaka 10 baadaye alirudi kwenye timu hiyo na kuisaidia Real Madrid kumaliza ukame wao wa miaka minne wa kushinda ubingwa wa La Liga baada ya kuwapa taji hilo 2007, lakini wiki chache baadaye alifukuzwa tena.

Marcello Lippi –Juventus

Marcello Lippi alishinda mataji matatu na Serie A na taji la pili la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika historia ya Juventus huko kwenye miaka ya tisini kabla ya kutimkia zake Inter Milan. Lippi aliinoa Juventus katika awamu mbili tofauti, kwanza ilikuwa kuanzia 1994 hadi 1999 na kurudi tena hapo Turin kuanzia 2001 hadi 2004. Huko Inter Milan alifukuzwa kazi na kurudi zake Juventus, ambako alikwenda kumbadili kocha Carlo Ancelotti. Katika awamu yake ya pili, Lippi aliwafikisha Juve fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2003 ambako walichapwa na AC Milan kwa mikwaju ya penalti.

Sir Matt Busby – Man United

Ukimweka kando Sir Alex Ferguson, kocha mwingine mwenye heshima kubwa huko Manchester United basi ni Sir Matt Busby. Kocha huyo mwenye heshima zake, amewahi kuinoa Man United katika awamu mbili tofauti, kwanza ilikuwa kuanzia mwaka 1945 hadi 1969 akaondoka, kisha alirudi kwenye timu hiyo mwaka 1970 na kudumu kwa mwaka mmoja tu. Busby alikuwa mmoja wa makocha bora kabisa wa soka waliowahi kutokea, ambapo alinusurika kifo kwenye ile ajali ya ndege ya Munich, Ujerumani mwaka 1958 iliyomaliza maisha ya mastaa kadhaa wa Man United. Alistaafu, kisha akarudi Old Traffold baada ya Wilf McGuinness kufukuzwa.

Jose Mourinho –Chelsea

Jose Mourinho alishinda mataji makubwa katika misimu yake yote mitatu ya mwanza aliyokuwa kwenye kikosi cha Chelsea kabla ya kurudi tena mwaka 2013 na kuendelea kufanya mambo yake. Kocha huyo Mreno, awamu yake ya kwanza kufanya kazi Chelsea ilikuwa kuanzia 2004 hadi 2007 alipofutwa kazi. Akarudi tena hapo mwaka 2013 na kufutwa kazi tena 2015 na kutimkia zake Manchester United alikofukuzwa tena. Katika awamu yake ya pili Mourinho alibeba ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2014, lakini kwenye kulitetea taji hilo msimu uliofuatia ndio hapo palikuwa pagumu na kujikuta akifunguliwa mlango wa kutokea.

Leonardo Jardim –AS Monaco

Kocha, Leonardo Jardim aliinoa AS Monaco kwa awamu mbili, ya kwanza ilikuwa kuanzia 2014 hadi 2018 kabla ya kufutwa kazi, kisha akarudishwa tena miezi minne baadaye. Kocha huyo aliongoza Monaco kubeba ubingwa wa Ufaransa mwaka 2017, lakini baadaye timu hiyo ilipoteza kundi kubwa sana la wachezaji wake muhimu na timu ikaishia kwenye nafasi ya pili kwenye ligi mwaka uliofuatia. Mambo yalikuwa magumu, akafutwa kazi na nafasi yake akachukua Thierry Henry. Lakini, hadi kufika Januari mwaka huu, Henry alifutwa kazi na Jardim akarudi kuchukua timu.

Claudio Ranieri – AS Roma

Mtaliano, Claudio Ranieri amepita kwenye timu nyingi, ikiwamo kuwapa Leicester City ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2016. Lakini, baada ya kupita huku na huko, hatimaye Ranieri amerudi Italia kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa AS Roma. Awamu yake ya kwanza kwenye kikosi hicho alikinoa kuanzia mwaka 2009 hadi 2011, huku akiwa na kumbukumbu ya kupokwa ubingwa na Jose Mourinho mwaka 2010 wakati huo alipokuwa akiinoa Inter Milan. Ranieri amerudishwa tena AS Roma mwaka huu na kumfanya awe kwenye orodha ya makocha waliorudi kwenye timu zao za zamani.

Makocha wengine

Makocha waliofanya hivyo orodha yao ni ndefu akiwamo Harry Redknapp aliyewahi kuinoa Portsmouth katika awamu mbili, Neil Lennon huko Celtic (2010-2014, 2019), Kevin Keegan (Newcastle, 1992-97, 2008), Louis Van Gaal (Barca, 1997-2000, 2002-03) na Luiz Felipe Scolari (Brazil, 2001-02, 2012-14)

Advertisement