Zidane aanza usajili wa beki wa Porto

Muktasari:

 

  • Real Madrid imefanya usajili wa kwanza ndani ya siku tatu tangu Zidane aliporejea kwa kumsajili beki wa Porto, Militao kwa pauni 43milioni

Madrid, Hispania. Real Madrid imemsajili beki wa kati wa Porto, Eder Militao ikiwa ni siku ya tatu tangu Zinedine Zidane aliporejea katika kikosi hicho.

Mfaransa huyo amerudi Madrid wiki hii baada ya kutimuliwa kwa Santiago Solari. Ameanza kusuka upya kikosi chake ili kuendana na kasi ya wapinzani wake wakubwa Barcelona na Atletico.

Leo Alhamisi wametangaza kumsajili beki chipukizi mwenye miaka 21, Militao kwa gharama ya pauni 43milioni kutoka Porto atajiunga nao msimu huu.

Militao amesaini mkataba wa miaka sita kucheza Bernabeu, huku Madrid wakithibisha kuwa nyota huyo atakaa katika klabu hiyo hadi 2025.

Miamba hiyo ya Hispania imeanza kutegenezwa upya chini ya Zidane, ambaye aliwaongoza kutwaa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa.

Zidane amejiunga na timu hiyo ikiwa nyuma kwa pointi 12 kwa vinara wa La Liga huku wakiwa na kumbukumbu ya kusambaratishwa vibaya nyumbani katika Ligi ya Mabingwa na Ajax katika hatua ya 16 bora.

Beki huyo amecheza mechi moja katika kikosi cha Brazil, anauwezo wa kucheza beki ya kati, kulia na kiungo mkabaji.

Chipukizi huyo alianza kucheza soka katika klabu ya Sao Paulo nyumbani kwao Brazil kabla ya msimu huu kujiunga na Porto.

Beki huyo tayari amefunga mabao matatu na kutegeneza mawili katika mechi 34 alizocheza akiwa na kikosi cha Portu jambo lililowavutia Madrid.

Uhamisho huo unakuja kukiwa na taarifa kuwa kiungo mchezeshaji wa Tottenham, Christian Eriksen ni miongoni wanaotakiwa na Madrid katika mpango wa Zidane wa kubadilisha Bernabeu.

Kama ilivyokuwa kwa Neymar, Kylian Mbappe na Eden Hazard wanaohusishwa kutakiwa na miamba hiyo ya Hispania kwa mujibu wa gazeti la AS, Eriksen naye yupo.