Ziara ya Sevilla ina manufaa mengi, tusiache fursa zitupite

Thursday May 16 2019

 

By Mhariri

WIKI ijayo Tanzania kwa mara nyingine tena inatarajia kupata ugeni wa kimataifa wakati klabu ya Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) itakuja nchini.

Msafara wa timu hiyo utakuja Tanzania kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kucheza pambano maalum la kirafiki la kimataifa kati yao na Simba litakalofanyika Mei 23 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Hii ni mara pili ndani ya miaka mitatu Tanzania kupata ugeni wa klabu kubwa barani Ulaya baada ya mwaka 2017, Everton iliyopo Ligi Kuu ya England (EPL), kuja nchini kwa ajili ya mechi ya kimataifa dhidi ya Mabingwa wa SportPesa Super Cup, Gor Mahia ya Kenya.

Ujio wa klabu hiyo ya Sevilla kama ilivyokuwa kwa Everton, unafanywa chini ya udhamini wa Kampuni ya SportPesa ambayo kwa kipindi kifupi tangu waingia Tanzania wamekuwa wakifanya mambo kadhaa makubwa katika sekta ya kijamii na michezo.

Ziara ya Sevilla inayoelezwa huenda ikaja nchini na zaidi ya msafara wa watu 70 ni kama neema kwa Tanzania kwani inaweza kuwa na faida kubwa kwa upande wa kiuchumi na michezo.

Kiuchumi, ziara hiyo inaweza kuliingiza taifa pato ya kigeni na pia kuitangaza nchi kitalii sambamba na kusaidia kuwaongezea kitu wadau wa soka wa Tanzania kujifunza kitu kupitia makocha, wachezaji na kadhalika.

Hivyo ni wakati wa kujipanga vizuri kuwapokea wageni hao tukiwa tumejipanga kwelikweli kuhakikisha ziara hiyo inaleta manufaa kama nchi na hata upande wa sekta ya michezo hususani soka.

Hakuna asiyejua Sevilla ni moja ya klabu kubwa nchini Hispania na hata Ulaya hasa kwa kufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Ulaya (UEFA Europe League) na kulitawala taji hilo kipindi ikiwa chini ya Kocha Unai Emery.

Ni timu inayoundwa na nyota mbalimbali wa kimataifa ambao wamekuwa wakizitibulia Barcelona ya Lionel Messi, Real Madrid na Atletico Madrid katika La Liga.

Kutokana na ubora wa timu hiyo kunaweza kuwa, ni sehemu nzuri kwa Simba kujifunza kitu kutoka kwa wageni hao kuanzia kwa benchi la ufundi, wachezaji na hata viongozi.

Kwa kuwa Sevilla inaendeshwa kisasa na imepata mafanikio makubwa Ulaya, ni wazi Simba iliyoingia kwenye mfumo mpya wa kujiendesha kisasa kwa njia ya hisa ni sehemu nzuri ya kujifunza kutoka kwa wenzao ili wafikie kule wanakokuota.

Pia kujumuika pamoja tu na klabu hiyo ni sehemu nzuri ya kuanzisha hata urafiki wa kisoka na kufungua milango ya wachezaji vijana wa Msimbazi kupata nafasi ya kwenda kujifunza katika klabu ya Sevilla kule Hispania.

Lakini kwenye suala la kiuchumi mbali na nchi kupata mapato ya kigeni kwa ujio huo na kuijitangaza kitalii, lakini pia ziara yao itawanufaisha wafanyabiashara, kitu ambacho kina tija kwa Watanzania kutokana na ziara hiyo inayoanza Mei 22.

Ingawa itakuwa ni ziara ya muda mfupi, lakini manufaa yake yakichangamkiwa yanaweza kuwa na maana kubwa kama ambavyo ilivyotokea kwa Everton walipokuja Tanzania mwaka juzi.

Mwanaspoti kama wadau wakubwa wa michezo na hususani soka tunaipongeza SportPesa kwa kuandaa ziara hiyo, lakini pia tukiikumbusha isiishie hapo tu, Watanzania walio wengi hasa mashabiki wa soka wangependa kuona timu mbalimbali zikija nchini.

Sio jukumu la SportPesa tu, lakini hata makampuni na wadau wengine wachangamke kuzileta timu za nje kwa ajili ya kuja kucheza kirafiki, kwani ziara zao zinakuwa na manufaa makubwa kwa nchini kuliko inavyotazamwa kama biashara ya mtu binafsi.

Kuja kwa klabu ama timu za nje sio tu, kunanufaisha nchini kiuchumi na pengine kisoka, lakini inachangia kuitangaza Tanzania nje ya mipaka, kwani kwa sasa huenda tangu ifahamike kuwa Sevilla inakuja nchini, mashabiki wa timu hiyo watakuwa wanaifuatilia Tanzania.

Kufuatiliwa huko sio tu kunachangia kuifanya Tanzania kufahamika, lakini pia inatangaza vivutio vingi vya kitalii vya nchi na mwishowe, hata baada ya Sevilla kuondoka mashabiki wao na hata wananchi wa Hispania watatamani kuja kuviona vivutio hivyo vya Kitalii.

Kubwa zaidi ni kwa Simba kujipanga kwa mchezo huo baada ya kupata fursa hiyo, ili kujitangaza na hata wachezaji wake kujitangaza mbele ya wageni wao na hivyo kufungua soko lao kwenda kucheza nje ya nchi.

Advertisement