Zesco wanatokaje? Mastaa Yanga kuvuna Sh 150 milioni

Muktasari:

Habari ambazo Mwanaspoti limezinasa ni kwamba, kama Yanga itaiondoa Zesco United na kusonga mbele, basi wachezaji watavuna zaidi ya Sh150 milioni.

YANGA imetua jijini Mwanza na kupokewa na mashabiki kibao kwa ajili ya kuweka kambi na kucheza mechi mbili za kirafiki.

Lakini, akili ya wachezaji, benchi la ufundi na mabosi wa klabu hiyo iko kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United.

Kama Yanga itapata matokeo mazuri kwenye mechi hizo mbili ikianzia nyumbani Septemba 14, mwaka huu, itafuzu kwa hatua ya makundi.

Mechi ya kwanza itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kisha kusafiri hadi Ndola, Zambia kumalizana na wapinzani wao hao wanaonolewa na kocha wao wa zamani, George Lwandamina.

Hata hivyo, katika kuhakikisha kuwa Yanga inapata matokeo mazuri na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo, mabosi kama kawaida wameweka mezani ahadi nzito ili kuona malengo yao ya kusonga mbele yanafanikiwa.

Habari ambazo Mwanaspoti limezinasa ni kwamba, kama Yanga itaiondoa Zesco United na kusonga mbele, basi wachezaji watavuna zaidi ya Sh150 milioni.

Hiyo ni mwendelezo wa ahadi za mabosi wa Yanga kwa wachezaji wao ambao kwenye mechi dhidi ya Township Rollers ya Botswana waliwapa bonasi ya Sh50 milioni ambazo tayari zimeshatolewa.

Sasa achana na hiyo, bosi mpya wa kamati ya mashindano ameibua jipya ambalo wachezaji kumbe wanajua.

Taarifa hizo zikathibitishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Rodgers Gumbo ambapo alisema wachezaji wametengewa Sh150 milioni.

Alisema wachezaji wote wanafahamu ahadi ya kitita hicho, hivyo jukumu la mwisho ni kwao kupambana ili kupata matokeo mazuri na kusonga mbele hatua ya makundi.

Gumbo alisema kuwa ahadi kamili ilikuwa Sh200 milioni, ambapo tayari Sh50 milioni zimeshatolewa kwa wachezaji. Hivi karibuni Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla alithibitisha kuwa wametimiza ahadi ya kuwapatia wachezaji fedha hizo ikiwa ni baada ya kuwang’oa Rollers.

“Tulipokuwa Botswana tuliwaambia vijana kwamba, tumewatengea motisha ya kutosha kama wataiondoa Rollers watachukua Sh50 milioni,” alisema Dk Msolla.

“Hilo wamelikamisha na siku hazikupita tatu ahadi hiyo imekamilishwa, lakini bado tuna kazi nyingine mbele dhidi ya Zesco United.

“Wakati ule tuliwaambia kama uongozi kiu yetu ni kuhakikisha tunafikia lengo la kutinga hatua ya makundi na ahadi kamili iliyopo ni Sh200 milioni. Kama tutafanikiwa kutinga makundi basi mzigo mwingine upo mezani unawasubiri.”