Zawadi nyingine za michezo ni bab’kubwa

Muktasari:

Hata hivyo, lipo kombe unaloweza kusema ni la aina yake na labda linahitaji mashine japo ndogo ya kunyanyua mizigo kulinyanyua ni lile la mchezo wa mieleka linalotumika kwa mashindano ya Sumo.

WASWAHILI wana msemo maarufu wa mcheza kwao hutuzwa. Hii ina maana yeyote yule ambaye amefanikiwa kufanya jambo zuri, basi hustahiki tuzo ili kuonyesha kuthaminiwa kwa mafanikio yake.

Hii pia ipo katika michezo mbalimbali. Katika miaka ya zamani ilikuwa ni kawaida kuona mshindi anapewa kombe au ngao na baadaye pakajitokeza mfumo wa hiyo zawadi ya kombe kufuatana na kitita cha fedha.

Siku hizi zipo zawadi za aina mbalimbali za michezo na ukisikia habari zake utashangaa na kubaki unacheka au kujiuliza hawa waliobuni zawadi hizo walikuwa na lengo gani.

Hata hivyo, katika zawadi zote hizi yenye gharama kubwa ambayo mshindi hukaa nayo kwa miaka minne na kurudisha, lakini akifanikiwa kuitia mkononi mara tatu mfululizo yaani katika kipindi cha miaka 12 ni Kombe la Dunia la kandanda.

Kombe hili lina urefu wa sentimeta 36.5 (inchi 14.4) na limetengezwa kwa dhahabu safi yenye uzito wa kilo tano (ratili 11). Thamani yake ni Dola 20 milioni.

Hata hivyo, lipo kombe unaloweza kusema ni la aina yake na labda linahitaji mashine japo ndogo ya kunyanyua mizigo kulinyanyua ni lile la mchezo wa mieleka linalotumika kwa mashindano ya Sumo.

Hili linaitwa Kombe la Waziri Mkuu na lina uzito wa zaidi ya kilo 40 na urefu wake ni futi tano na inchi tano. Mshindi hukabidhiwa kikombe kidogo kinachofanana na hilo kombe na halisi likiwa pembeni.

Kombe jingine kubwa ni la mashindano ya mbio za magari yajulianayo kama Daytona 500. Kombe hili lina uzito wa ratili 54.

Kitu cha aina yake kilichopo katika kombe hili na sijui kwa nini ikawa hivyo ni kuwepo umbile la mwanamume akiwa mtupu (hana nguo) akipepea bendera.

Lakini zipo zawadi za kuchekesha. Kwa mfano, kule Jamaica zawadi nyingi zinazokusudiwa kuwa ndio kombe la ushindi huwa na umbile la ndizi kuonyesha umuhimu wa chakula hiki kwa watu wa kisiwa hiki cha Carribbean.

Katika mashindano ya shule kwa michezo mbali mbali makombe ya washindi huwa tafauti na haya tunayoyaona hapa kwetu. Yapo ya kobe, konokono, kaa, chura, mamba na vitu vya ajabu ajabu.

Katika mashindano ya tenisi ya kampuni ya gari za aina ya Volvo za Sweden moja ya zawadi maarufu ina muundo wa chombo cha kumwagia taka kama vile tunavyoviona kwenye ofisi mbalimbali.

Katika baadhi ya nchi na hasa Uingereza na Marekani mashindano ya kampuni zinazoshughulikia kutengeneza vifaa vya usafi wa nyumbani na mazingira hutoa zawadi yenye umbo la choo.

Baadhi ya hivi vyoo vyenye umbo la kobe huwa na uzio wa kilo tano hadi sita.

Katika mashindano ya baadhi ya shule za Marekani na India mshindi hushinda zawadi yenye umbo la shoka, msumeno au nyundo.

Sijui huu mtindo wa kutoa vikombe na zawadi za ajabu ajabu kwa washindi wa mashindano mbalimbali ukianza hapa kwetu tutashudia vikombe vyenye umbo la aina gani. Ni vyema tukavuta subira, lakini si ajabu hata kidogo tukawa na zawadi za sanamu la kama la kakakuona, fisi, bata mzinga au za mfano wa Mlima Kilimanjaro.

Wakati ndio utaokaotupa jawabu sahihi ni zawadi za aina gani tunazoweza kuziona kwenye viwanja vyetu.

Tusubiri kwani tunaambiwa… Mambo kangaja huenda yakaja.