Zali la Lionel Messi Barca

Muktasari:

Huu hapa, utatu matata Messi aliyowahi kucheza nao huko Barcelona katika kipindi chote cha maisha yake ya soka.

BARCELONA,HISPANIA.KAMA kuna mtu ana zali kwenye dunia ya soka, basi ni supastaa Lionel Messi linapokuja suala la kuichezea Barcelona.

Mwanasoka huyo mshindi mara tano wa Tuzo ya Ballon d’Or, kwa kipindi chake chote cha maisha ya soka aliyoitumikia Barcelona, amepata bahati ya kucheza sambamba na washambuliaji hodari duniani na kutengeneza kombinesheni matata ya mafowadi watatu.

Kwa msimu ujao wa 2019/20 huko kwenye La Liga, Messi atapata nafasi ya kutengeneza utatu mwingine moto kwenye kikosi hicho ambao utaundwa na Antoine Griezmann na Luis Suarez baada ya wababe hao wa Nou Camp kumnasa fowadi wa Atletico Madrid katika dirisha hili la majira ya kiangazi.

Hilo litakuwa zali jingine kubwa kwa Messi kutokana na kupata bahati ya kucheza fowadi zenye mastaa wote wakali.

Huu hapa, utatu matata Messi aliyowahi kucheza nao huko Barcelona katika kipindi chote cha maisha yake ya soka.

5. Thierry Henry - Samuel Eto’o - Lionel Messi

Wakati Ronaldinho alipoondoka Barcelona kwenda kujiunga na AC Milan mwaka 2008, staa wa soka kutoka Ufaransa, Thierry Henry alichukua nafasi huko Nou Camp na kwenda kucheza kwenye kombinesheni ya fowadi watatu moto sambamba na Lionel Messi na Samuel Eto’o.

Katika msimu wa 2008/09, fowadi hiyo ya mastaa watatu maarufu, iliisaidia Barcelona kubeba ubingwa wa La Liga, Copa del Rey na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuichapa Manchester United kwenye mchezo wa fainali huku kwenye benchi kocha wao, alikuwa Pep Guardiola.

4. David Villa - Lionel Messi - Pedro

Msimu wa 2010-11 uliwashuhudia David Villa na Pedro waliwekwa kwenye fowadi ya Barcelona na kucheza na Lionel Messi kwenye utatu wa aina yake kwenye kikosi hicho.

Kwa msimu huo, Kocha Pep Guardiola aliamua kumtumia Messi kama namba 9 bandia, huku Villa akicheza upande wa kushoto na Pedro alikuwa akitokea upande wa kulia. Katika msimu huo, Pedro alikuwa akifanya dhambi zote kuhakikisha Messi na Villa wanafanya mambo yao. Hakika, Messi alikuwa kwenye ubora mkubwa sana na Barcelona ilibeba La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuthibitisha kwamba fowadi yake ya wakali watatu ilikuwa moto.

3. Thierry Henry - Zlatan Ibrahimovic - Lionel Messi

Barcelona ilifanya uamuzi wa kumchukua Zlatan Ibrahimovic mwaka 2009 na kumwaachia straika Samuel Eto’o aende Inter Milan. Uhamisho huo ulikuwa wa kishindo, ambapo Kocha Pep Guardiola alifanya kutengeneza kombinesheni ya wakali watatu kwenye fowadi yake, ambapo Ibrahimovic alikuja kuungana na Thierry Henry na Lionel Messi.

Hata hivyo, Guardiola alipata shida kidogo kwenye kuimudu staili ya uchezaji ya supastaa wa Sweden, Ibra.

Kutokana na hilo baadaye aliamua kumtumia kama mbadala wa Lionel Messi na hivyo kuufanya utatu huo usipate muda wa kutosha wa kucheza pamoja.

2. Lionel Messi - Luis Suarez - Neymar

Bila shaka moja kati ya utatu matata kabisa uliowahi kutoka kwenye soka unaocheza kwenye nafasi ya ushambuliaji.

Barcelona ilibahatika kuwa na kombinesheni hiyo iliyokuwa ikiundwa na Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar iliyoanza kucheza pamoja kwenye msimu wa 2014/15, ambapo ilibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Pacha hiyo iliyokuwa ikifahamika kwa jina la MSN na hakika ilikuwa moto kila ilipokaribia goli, asikwambie mtu makipa wa timu pinzani waliteseka sana. Ndiyo iliyofanya maajabu kwenye kupindua matokeo dhidi ya PSG kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2017/18 baada ya kufungwa 4-0 kisha ikashinda 6-1.

1. Ronaldinho - Samuel Eto’o - Lionel Messi

Wakati Lionel Messi alipoanza kuibukia kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona, alitengeneza kombinesheni matata kabisa kwenye sehemu ya ushambuliaji na wakali wengine wawili, Ronaldinho na Samuel Eto’o.

Messi alicheza upande wa kulia, Ronaldinho kushoto na Eto’o alisimama kati kwenye fowadi hiyo moto ya wakali watatu.

Kipindi hicho Messi ndio kwanza alikuwa akichipukia hivyo alikuwa akipishana kikosini na Ludovic Guily.

Licha ya kwamba hakupewa nafasi sana kipindi cha Kocha Frank Rijkaard, lakini Messi aliisaidia Barcelona kubeba La Liga, Supercopa de Espana na Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2006.