Zahera wala hana presha

MKURUGENZI wa Ufundi wa Gwambina FC, Mwinyi Zahera amesema mbali ya kushindwa kupata pointi katika michezo minne ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, bado hana wasiwasi katika timu hiyo kwa vile anajua ugeni wa vijana wao katika ligi utaondoka na watafanya kweli.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga, alisema timu yao ndio kwanza inacheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, hivyo wakati mwingine wanaangushwa na uzoefu, lakini anaamini wakishaizoea watakuwa moto kwa sababu timu yo ina vijana wenye uwezo mkubwa kisoka.

Alisema kwa namna alivyokiangalia kikosi chake anaamini kinahitaji wachezaji wanne mpaka wa tano wapya wenye uzoefu wa ligi, kazi inayoweza kufanywa kwenye dirisha dogo.

“Wachezaji hao wapya ambao nitawaleta hapa inaweza kuwa wa raia wa kigeni na wengi watakuwa ni mastraika kwani timu yetu nimegundua kuna tatizo kwenye kumalizia,” alisema.

“Usajili huo ambao tutaufanya si kwa wachezaji wa nje tu bali hata kuna watakaokuwa wamefanya vizuri kwenye ligi ya ndani tunaweza kuwachukua kwenye dirisha dogo,” alisema Zahera aliyeuzungumzia mchezo wao dhidi ya Simba na kusema; “Tulizidiwa katika maeneo mengi, ila kwenye mechi tatu za awali tumecheza vizuri.”