Zahera mbishi, awagomea mabosi TFF

Muktasari:

Kocha huyo, alisema ni ngumu kuwa na ushindi wa kutosha kwenye Ligi kama kuna kuwa na wimbi kubwa la viporo ambavyo kwa namna moja ama nyingine vinatafsiriwa vibaya.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera mbishi kinoma. Akiwa bado hajajua hatma ya kesi yake aliyoburuzwa Kamati ya Nidhamu na Maadili, ameendelea kuwachana tena TFF.

Mkongoman, huyo amesisitiza hatanyamaza kusema ukweli kwa kitu anachokiona akiendi sawa na kusema idadi kubwa ya viporo alivyokuwa nao Simba ni mambo yaliyopunguza ushindani na kutengeneza bingwa wa msimu huu.

Alisema hawezi kunyamaza wakati ukweli ndivyo ulivyo na kudai vi vyema tu TFF ikawapa tu Simba taji lao kwao Yanga haina nafasi kwa vile wenzao wana mechi nyingi mkononi.

Kocha huyo, alisema ni ngumu kuwa na ushindi wa kutosha kwenye Ligi kama kuna kuwa na wimbi kubwa la viporo ambavyo kwa namna moja ama nyingine vinatafsiriwa vibaya.

“Sioni kama tuna nafasi ya kuchukua ubingwa tena, tumebaki na michezo miwili wakati wenzetu wanamichezo mitano, hii ni mbaya sana, inaua soka la Tanzania, hivyo nilishajitoa katika mbio za ubingwa tangu Simba walipocheza na Mazembe.”

“Soka lenu linaelekea kubaya, namna hii ya upangwaji wa ratiba, inaweza kuathiri pia viwango vya wachezaji wengi wanaocheza Ligi ya ndani kwenye kikosi cha timu ya taifa,” alisema kabla ya kuongeza

“Kuna kipindi Yanga ilicheza mechi 15 huku timu nyingine zikicheza mechi saba, sio sawa kabisa, mbona kuna Ligi za mataifa mengine ambayo yapo hapa hapa Afrika lakini hakuna matatizo ya ratiba na timu zao zimekuwa zikishiriki kwenye mashindano ya kimataifa,” alisema kocha huyo.

“Nimeipenda Ligi ya Afrika Kusini, siku ya mwisho ndio iliyotumika kutangazwa bingwa wa msimu huu, nilipenda na hapa hata kama atatangazwa mapema isiwe kwa kisingizio cha ratiba iwe kwa kuzidiwa uwezo.”

Zahera na wanamichezo wengine nane walishtakiwa na Bodi ya Ligi kwa makosa ya utovu wa nidhamu ambapo Jumapili iliyopita kamati ilikutana kuwasikiliza na hukumu zao hazijatoka.