Zahera hamchukii Ajibu, anamtaka asikombe mboga ili ashibe

WAKATI, Sepp Blatter anakumbwa na matatizo ndani ya Ofisi Kuu za Fifa, rafiki yake wa karibu, Michel Platini, alimtaka ajiuzulu kwa manufaa ya taasisi husika.

“Blatter ni rafiki yangu wa karibu sana. Mimi ndiye niliyemsaidia kushinda urais wa Fifa 1998.

Lakini, kutokana na mambo yaliyotokea Fifa, namsihi ajiuzulu. Ni vizuri kumwambia ukweli rafiki yako. Kama kuna kitu cha kumsaidia rafiki yako basi ni kumwambia ukweli.”

Ukweli huu wa Platini ndio ninaouona kwenye kinywa cha Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera kwa Ibrahim Ajibu.

Baada ya mchezo wa Simba na Yanga, Septemba 30 mwaka huu, Zahera alinukuliwa akisema hafurahishwi na uelewa wa wachezaji wake kadhaa juu ya mchezo, hasa wanapobadili mbinu za mchezo.

Zahera alisema amekuwa akicheza na wachezaji 9 hadi 8 kwa mchezo, huku waliobaki wakiwemo uwanjani kimwili lakini kimchezo hawapo.

Alisema kila anapobadili mbinu za mchezo kutokana na mahitaji ya mechi husika, kuna wachezaji wawili hadi watatu hujikuta wakishindwa kuielewa mbinu mpya hivyo kujikuta akicheza na wachezaji 9 hadi 8 walielewa, kwa kila mchezo.

Kwa mechi ya Simba na Yanga, mchezaji ambaye hakuelewa alichokitaka Zahera, alikuwa Ibrahim Ajibu na akasema ndio maana alilazimika kumtoa kwa faida ya timu na kulinda heshima yake bila kujali wapenzi wa timu hiyo wanamtazama vipi.

Oktoba 20, kwenye mchezo dhidi ya Alliance FC, Ajibu alifunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao na kuisaidia timu yake kushinda 3-0, lakini haikutosha kwa Zahera.

Baada ya mchezo huo, Zahera akampa Ajibu alama 4/10 akisema hawezi kumpa alama zaidi ya hizo kwa sababu haitoshi tu kufunga na kutoa pasi za mabao, anahitaji zaidi ya hapo uwanjani.

IBRAHIM AJIBU

Ajibu ni mchezaji anayefurahisha kumtazama uwanjani. Anaufanya mchezo mgumu wa soka uonekane rahisi sana.

Msimu huu, amehusika na mabao 11 kati ya mabao 14 yaliyofungwa na timu yake inayofundishwa na Zahera.

Kwa mtazamo rahisi usiohitaji hata cheti cha elimu ya msingi kuelewa ni kwamba Ajibu ndiye mchezaji bora zaidi wa Yanga msimu huu.

Lakini kwa Zahera, Ajibu hajafanya vya kutosha, anamtaka afanye zaidi na hapo kutamfanya kuwa bora zaidi.

Hapa ndipo utakumbuka ule msemo wa Kiswahili kwamba; ‘Anayekukataza kukomba mboga, anataka ushibe!’

Ni kwamba Zahera anamuona, Ajibu kama mchezaji anayeweza kufanya zaidi ya anavyofanya sasa akiongeza juhudi na usikivu.

Kwa kuwa Zahera ndiye anayekaa na Ajib mazoezini tofauti na watu wengine ambao, wanamuona Ajibu ndani ya dakika 90 pekee, ndiye anayemjua mchezaji huyo. Hivyo anaposema haridhiki na mchango wake kwenye timu, anajua anachomaanisha.

Ni wajibu wa Ajibu kuyafanyia kazi mawazo ya kocha wake ili afike mbali zaidi ya hapa alipo sasa. Asihadaishwe na sifa za mashabiki ambao huwa hawaangalii mchezo kiufundi kama anavyofanya kocha.

Ukirejea alichokisema Zahera baada ya mchezo dhidi ya Simba, utagundua kwamba Ajibu ana safari ndefu.

Haiwezekani mchezaji wa daraja kama lake akashindwa kuelewa maelekezo ya mwalimu. Anatakiwa alifanyie kazi hilo kwanza halafu mengine yatafuata.

Zahera anamtakia mema Ajibu, ndio maana licha ya kumkosoa mara kwa mara, bado anampa nafasi kila mchezo.

Asimchukie kocha wake, badala yake, ayafanyie kazi mambo yote anayoambiwa ili asonge mbele.