Zahera awavaa waamuzi kipigo cha Yanga

Saturday May 11 2019

 

By Thomas Ngitu, Mwananchi

Dar es Salaam.Timu ya Biashara United imetumia vyema uwanja wake wa nyumbani, baada ya kuilaza Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliotawaliwa na vurugu.

Wachezaji wa timu zote mbili walionyeshana ubabe kwa dakika zote 90 za mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Karume ambao Biashara ilishinda bao 1-0.

Mara kwa mara mchezo huo ulikuwa unasimama baada ya wachezaji wa timu zote mbili kuvaana wakitaka kuzipiga katika matukio tofauti.

Mwamuzi wa mchezo Daniel Warioba wa Mwanza alishindwa kutoa adhabu mapema licha ya wachezaji wa timu hizo kukosa nidhamu ya mchezo.

Warioba alitoa kadi nyekundu dakika ya 90 kwa nahodha wa Biashara Lenny Kisu kwa mchezo mbaya.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alidai timu yake imefungwa kutokana na uamuzi mbovu aliodai ulichangiwa na mwamuzi huyo.

Advertisement

“Nilitumiwa barua na Bodi ya Ligi kwa kutoa maneno kama haya, lakini siwezi kuficha, hii ni aibu kama soka itaendelea hivi hatuwezi kufika mbali. Angalia lile bao lilikuwa sahihi kweli? Alihoji Zahera.

Kocha wa Biashara Amri Said alisema waliisoma Yanga ilipocheza mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Lipuli ya Iringa waliofungwa mabao 2-0.

“Niliisoma Yanga ilipocheza na Lipuli, inatumia mipira mirefu. Nilitoa maelekezo kwa wachezaji wangu kudhibiti mbinu yao. Inawezekana mwamuzi ana kasoro kama binadamu, lakini kwangu naona amefanya vizuri,” alisema Said.

Kwa matokeo hayo Biashara imefikisha pointi 40 katika msimamo wa ligi na Yanga imebaki katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 80.

Mchezo wenyewe

Yanga ilianza mchezo kwa kasi huku ikitumia mipira mirefu kupeleka mashambulizi na mara chache Biashara ilijibu kwa kutumia viungo wa pembeni.

Dakika nane za mwanzo zilikuwa za mashambulizi kwa timu zote mbili na Biashara ilipata faida baada ya kupata bao la kwanza dakika ya tisa lililofungwa na mshambuliaji Tariq Kilakala.

Kilakala alifunga bao baada ya kupata mpira wa krosi uliopigwa na Wilfred Nkouluma na mabeki wa Yanga walizembea kumbana mfungaji wakidhani ameotea.

Yanga ilizinduka kusaka baola kusawazisha, lakini mipango ilivurugwa kutokana na hali ya uwanja kutokuwa katika kiwango bora kufuatia mvua mkubwa iliyokuwa ikinyesha.

Mshambuliaji wa Yanga, Herieter Makambo alikosa nafasi za kufunga licha ya kuingia katika eneo la hatari.

Biashara ilikosa bao dakika ya 22 baada ya George Makanga kuwatoka mabeki wa Yanga, lakini alipiga kiki iliyotua mikononi mwa kipa Klaus Kindoki.

Mara kwa mara safu ya ulinzi ya Yanga hasa mabeki wa kati Andrew Vicent na Kelvin Yondani kutokuwa na maelewano mzuri wakati mashambulizi yanapoelekezwa langoni mwao.

Kwa takribani dakika zote za kipindi cha kwanza Biashara ilionekana kuwa imara katika safu ya ushambuliaji kupitia kwa akina Innoecent Edwin na Kilakala waliokuwa wakiitoka mara kwa mara ngome ya Yanga.

Dakika 50 Makambo alikosa utulivu ambao ungeipa bao Yanga baada ya kupiga mpira wa kichwa kutokana na faulo iliyopigwa na Thabani Kamusoko, lakini mpira ulitoka.

Yanga ilifanya mabadiliko dakika ya 58 kwa kuwatoa Rafael Daud na Mohammed Issa na nafasi zao zilichukuliwa na Deus Kaseke na Mrisho Ngassa ambao waliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Biashara.

Makambo alikosa bao dakika ya 74 baada Haji Mwinyi kupiga mpira wa krosi ambao mchezaji huyo alishindwa kufunga licha ya kuingia katika eneo zuri.

Biashara United: Nurdin Barola, Kauswa Benard, Mpapi Nasibu, Wilfred Nkouluma, Lameck Chamkaga, Lenny Kisu, Juma Mpakala, Derick Kiakala, George Makanga na Inocent Edwin.

Yanga: Klaus Kindoki , Paul Godfrey, mwinyi Haji, Andrew Vicent, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko, Mohammed Issa, Papy Tshishimbi, Herieter Makambo, Amis Tambwe na Raphael Daud.

 

Advertisement