Zahera awaka, awashukia Ngassa na Kaseke

Muktasari:

  •  Kiwango wanachokionyesha mawinga wa Yanga, Mrisho Ngassa na Deus Kaseke, kimemfanya kocha wa timu hiyo kuwaza kusajili winga mwingine


BAADA ya matokeo sare ya 1-1 waliyoyapata Yanga dhidi ya Ndanda FC juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Kocha mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera amefunguka kama kuna eneo linamkwamishia mipango yake, basi ni viungo wa pembeni.

Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera alisema upande wa viungo hao umekuwa na changamoto kubwa na unamwangusha kutokana na wachezaji kutokuwa na kile ambacho anakihitaji kukiona katika mechi zake.

“Kweli inawezekana Kaseke kiwango kimeshuka, ndio maana anatokea nje, lakini hata Ngassa na Rafael bado hawajafanya kitu ambacho nahitaji kukiona katika wachezaji wangu kwenye namba ile, bado naweza nikafanya kitu dirisha dogo, naweza kuleta mtu mwingine,” alisema.

Akizungumzia kuhusu kutoka katika kinyang’anyiro cha mbio za ubingwa, alisema bado ana nafasi kubwa ya kuendelea kupambana na sio muda sahihi wa kukata tamaa.

“Tumetoka sare mbili na bado tuna mechi nyingi mbele, sijapoteza kujiamini katika mechi zangu labda kama ningefungwa mabao zaidi ya sita, bado ligi inaendelea,” alisema na kuongeza, wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi lakini wanashindwa kuzitumia.