Zahera atoa ramani ya vita

Muktasari:

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera jana jioni alianza program ya kujiweka fiti kwa ajili ya kuwakabili wapinzani ambao, walitoka sare kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

HATUA ya Yanga kuingiza jeshi lake mapema ndani ya Jiji la Gaborone, Botswana kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano na Township Rollers ni kama kumewashtua wapinzani wao.

Mchezo huo utapigwa Jumamosi huku Yanga ikiwatanguliza mapema kabisa mabosi wake, Makamu Mwenyekiti Frederick Mwakalebela na yule wa Kamati ya Mashindano, Rodgers Gumbo.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera jana jioni alianza program ya kujiweka fiti kwa ajili ya kuwakabili wapinzani ambao, walitoka sare kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kazi inayofanywa na benchi la ufundi chini ya Zahera kwa sasa ni kukiweka sawa kikosi chake tayari kwa mchezo huo. Mipango ya kuhakikisha ushindi unapatikana ili kupata nafasi ya kusonga mbele katika mchezo huo wa ugenini.

Hata hivyo, imebainika kwenye mechi mbili za kirafiki ambazo Yanga ilicheza dhidi ya Polisi Tanzania na kulala kwa mabao 2-0 kisha AFC Leopard ya Kenya, bado Zahera alikuwa akipima ubora wa kikosi chake kwa ajili ya kujipanga dhidi ya Rollers.

Kwenye mchezo dhidi ya Polisi, Zahera aliwatumia wachezaji ambao wamekuwa hawapati namba mara kwa mara huku pia akiwatumia waliopo kwenye kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, kikosi ambacho alikitumia kwenye mchezo dhidi ya AFC Leopards ndicho kinatajwa, kitakwenda kuikabili Rollers.

Baadhi ya viongozi na mashabiki wa Yanga wanaamini, kama Zahera atashusha mziki huo basi shughuli uwanjani itakuwa nzito na uwezekano wa Yanga kupindua matokeo ni mkubwa.

Ukuta uwe hivi

Kwenye ukuta wa Yanga ambao kwa sasa unatajwa kuwa umepata nguvu kutokana na kurejea kwa beki Kelvin Yondani, langoni atasimama kipa namba mbili Metacha Mnata.

Yanga haitakuwa na Farouk Shikalo, ambaye bado hajapata leseni ya kuichezea klabu yake kwenye michuano ya Caf, lakini kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza, Mnata atalinda lango huku akipewa ulinzi na mabeki wanne.

Kwa mujibu wa hesabu zilizokubalika ni kwamba, ukuta wa Zahera unaweza kuanza na mabeki wote walioanza na kumaliza mechi ya FC Leopards, ambapo kwa kulia atakuwa Paul Godfrey ‘Boxer’ kushoto ni Ally Sonso huku mkongwe Kelvin Yondani na Lamine Moro wakisimama pamoja katikati.

Kwa staili ya uchezaji wa washambuliaji wa Rollers wakiongozwa na Segolame Boy, Motsheletsi Sikele na Ivan Ntege watakuwa na kazi nguvu kuipenya ngome ya Yanga kama watakuwa wametumia siku chache kujiweka sawa na kucheza kwa maelewano.

Lakini, Mwanaspoti linafahanu kuwa kesho Zahera atawakusanya tena vijana wake akiwafungia na kuwasoma Rollers katika mchezo uliopita huku wakiangalia mechi zingine mbili walizonasa wakiwa ndani ya Gaborone.

Kiungo kati

Eneo la katikati Yanga inaonekana kuimarika zaidi kutoka na nahodha wake, Papy Kabamba Tshishimbi kuwa kwenye kiwango bora sambamba na Mohamed Issa ‘Banka’ ama Feisal Salum Fei ‘Toto’ ambao watacheza pamoja.

Mwanaspoti ambalo linafuatilia kila kinachoendelea kwenye kambi ya Yanga, jana Zahera alitumia muda mwingi kumpa nafasi Fei Toto huku akiwajaribu viungo wote watatu kuanza pamoja.

Hata hivyo, Yanga wanaweza kukutana na wakati mgumu kama watashindwa kucheza lkwa kuelewana na kupoteza mipira kila wakati kama ilivyokuwa kwenye mechi zilizopita.

Katika mchezo dhidi ya Kariobang Sharks, eneo la kiungo la Yanga lilionekana kuwa imara huku Banka akicheza soka la kiwango cha juu.

Viungo wa Rollers wakiongozwa na Galabgwe Moyana, Edwin Moalos, Boyo Lecheana na Ofentse Nato ni wazuri katika kukaba na kupandisha mashambulizi langoni mwa adui.

Wamekuwa na staili ya uchezaji wa kupiga pasi fupi fupi na wakati mwingine ndefu wanapokwenda kushambulia langoni mwa adui huku walinzi wake wakisogea juu kwa ajili ya kukabiliana na mipira ya mashambulizi ya kushtukiza.

Hapa ndio kazi

Mwisho wa matatizo ndio hapa, ambapo katika mechi za majaribio zilizopita licha ya Yanga kuibuka na ushindi, lakini bado eneo hilo halijaonekana kukaa sawa.

Kumekuwepo na matatizo katika kumalizia nafasi za mwisho na washambuliaji wa Yanga bado hawana muunganiko mzuri.

Hata hivyo, kiongozi mmoja wa Yanga amezungumza na Mwanaspoti na kueleza, tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi wakiwa kambini na sasa ni kuonyesha makali tu uwanjani.

Inaelezwa kwamba, kama Zahera ataanza na viungo hao watatu basi huenda Sadney Urikhob akaanzia benchi ili kumuacha Mapinduzi Balama, Juma Balinya na Patrick Sibomana kusimama jirani na lango la adui kutafuta mabao.

Hata hivyo, nguvu ya kikosi hicho itakuwa pia kwa Urikhob, mkongwe Mrisho Ngassa, Deus Kaseke na hata Issa Bigirimana ambao wamekuwa wakijaribiwa ingawa nafasi yao ya kuanza ikiwa ndogo.