Zahera asimulia alivyokosa mamilioni

Muktasari:

Tukio hilo lilitokea juzi usiku wakati wa tafrija ya kufuturisha wadau wa klabu hiyo na wachezaji wa kikosi hicho katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera ameangua kilio mbele ya wadau wa soka wakati akisimulia safari yake ya kujiunga na klabu hiyo kongwe nchini.

Zahera alishindwa kujizuia kutoa machozi hadharani alipokuwa akieleza namna alivyokacha mamilioni ya klabu ya Buildcon ya Zambia iliyomuahidi kumpa mkataba mnono.

Tukio hilo lilitokea juzi usiku wakati wa tafrija ya kufuturisha wadau wa klabu hiyo na wachezaji wa kikosi hicho katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Serena, Dar es Salaam.

Zahera alisema wakati akiwa DR Congo Buildcon ya Zambia yenye nguvu ya fedha ilikuwa ikitafuta kocha mkuu baada ya kuwatimua makocha wake watatu raia wa Hispania.

Alisema mmiliki wa klabu hiyo aliwasiliana na mdhamini mkuu wa jezi ya timu ya Taifa la Congo ambaye alimpendekeza Zahera kwenda kujaza nafasi Buldcon.

“Mmiliki wa Buildcon anajuana na mdhamini wa jezi ya timu ya Taifa ya Congo aliambiwa atafute kocha mzuri nikashangaa aliniambia Buildcon wanatafuta kocha mzuri, nikamuuliza wewe unadhani mimi ni kocha mzuri?” alisimulia Zahera kwa hisia.

Zahera alisema alitumiwa tiketi kwenda Zambia na mmiliki wa Buildcon alimuuliza anataka kiasi gani ili ampe mkataba wa kuifundisha timu hiyo ya Ligi Kuu Zambia.

“Tajiri wao aliniambia niseme ni kiasi gani nahitaji nisaini mkataba nikamwambia mimi si mtu wa kuhitaji fedha sana wakati huo hawajashinda hata mechi moja na siku mbili mbele wanacheza mechi ngumu ya ligi na Zanaco.

Zahera alisema katika mchezo huo walitoka sare, lakini mmiliki huyo aliongeza kasi na kufanya naye mazungumzo ili atie saini mkataba wa kuendelea na kazi.

“Sikuwa nakaa kwenye benchi kwa kuwa nilikuwa na mkataba na Congo, lakini tuliongea kuhusu mkataba tukakubaliana. Lakini siku moja kabla ya kwenda kusaini mdogo wangu pekee katika familia yetu alinipigia simu akaniuliza niko wapi ?Nikamwambia nipo Zambia kuna timu niko nayo akaniambia nisiingie nayo mkataba anataka nije Tanzania.

“Nikamwambia mbona hapa Zambia hawa jamaa nimeshaongea nao kila kitu na natakiwa nisaini nao mkataba?Akanijibu nisisaini anataka nije Tanzania nisaini Yanga nikamwambia mbona hiyo timu siijui?.

Zahera alisema klabu pekee alizokuwa akizijua kwa umaarufu ni TP Mazembe, Al Ahly, Esparance kwa kuwa alikuwa akiishi Ulaya kwa miaka 40.

“Unajua huyu ni mdogo wangu pekee tumebaki wawili tu baada ya baba na mama yetu kufariki (anaanza kulia). Mdogo wangu na Hussein Ndama walinitumia tiketi, nikawaambia wale jamaa (Buildcon) wasubiri nije nchini mara moja,” alisema Zahera.

Kocha huyo alisema baada ya makuliano na Yanga alianza kazi na aliikuta Yanga ikijindaa kwenda kambini mkoani Morogoro.

Katika mazungumzo hayo, Zahera aliunga mkono kauli ya msanii Steve Mengele ‘Steve Nyerere aliyesema Yanga ina mashabiki wengi, lakini wanaokwenda uwanjani ni wachache.

“Yanga ukipita huku na kule kuna mashabiki wengi, lakini ukija uwanjani huwaoni sababu gani hawaji uwanjani? Timu yao inacheza ligi inashinda, tunashinda mechi mpaka 30 lakini watu hawaji uwanjani.

“Nawapongeza sana wachezaji wangu wamecheza ligi wakiwa na maisha magumu sana lakini wamekuwa wakinisikiliza kama sio kudhulumiwa mechi kama tano leo (juzi) tungekuwa mabingwa msimu ujao,”alisema Zahera. Yanga inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 83.