Zahera amtikisa kigogo Simba

Muktasari:

  • Makamba aliyasema hayo wakati Yanga ya Zahera ikiwa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 74 katika mechi 32 ilizokwishacheza ikifuatiwa na Azam na Simba ambayo ina pointi 63 katika mechi 25 walizocheza.

KASI ya Mwinyi Zahera wa Yanga katika Ligi Kuu Bara, imemtikisa hadi kigogo mmoja mzito wa Simba akidai kama sio kocha huyo watani zao wangepata tabu sana na kusisistiza kwa morali aliyonayo Mkongomani huyo imemfanya hadi yeye kupatwa mdadi na kuahidi kuichangia fedha klabu hiyo.

Lakini wakati kigogo huyo akiweka msimamo wake huo kwa Yanga, kocha huyo amesisitiza katika mechi zao sita zilizosalia atakomaa kuhakikisha Simba yenye kuwategemea kina Meddie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi hawatetei taji la Ligi Kuu Bara msimu huu.

Sikia sasa. Kiwango cha kocha Zahera kimemvutia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, January Makamba ambaye ni mwanachama na mshabiki mkubwa wa Simba.

Makamba alisema kocha huyo ameweza kurejesha morali ya timu licha ya changamoto wanazopitia kwa sasa na anafurahishwa mno na hali hiyo, huku akisisitiza kuwa angependa kuona Yanga ikiwa imara ili kuifanya Simba izidi kukimbilia mafanikio na kwamba yu tayari kuichangia fedha Jangwani.

Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Makao Makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam jana Jumatano, Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli alisema, kocha Zahera amefanya kazi kubwa ya kujenga nidhamu ya timu.

“Pamoja na changamoto ambazo Yanga inapitia, lakini timu inapambana, wachezaji wana nidhamu na wanacheza kwa jezi za klabu yao,” alisema Makamba.

Alisema Yanga imekuwa tofauti, wachezaji wana morali, licha ya kupitia kipindi kigumu ikiwamo kusotea mishahara yao.

“Binafsi nitaichangia Yanga si chini ya Sh I milioni, hakuna Simba imara bila Yanga imara, Simba hatupaswi kuikejeli Yanga kwa kipindi inachopitia, tujifunze kutokana na changamoto zote wanazopitia, wanacheza mpira na wanapigania ubingwa,” alisema Makamba.

Makamba aliyasema hayo wakati Yanga ya Zahera ikiwa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 74 katika mechi 32 ilizokwishacheza ikifuatiwa na Azam na Simba ambayo ina pointi 63 katika mechi 25 walizocheza.

“Zahera anastahili ‘credit’ amefanya kazi kubwa kurejesha nidhamu na morali kwenye timu,” alisema.

SIMBA FRESHI

Kuhusu Simba, akizungumzia uwekezaji wa Simba na matokeo ambayo timu inayapata, Makamba alisema thamani ya uwekezaji ndani ya Msimbazi imeonekana, lakini tatizo lililopo wamebadili mfumo lakini mizizi ya utamaduni wa zamani bado upo.

“Structure ya uendeshaji wa klabu imebadilika, lakini culture bado iko pale pale, wanapaswa kwanza kuondoa mambo ya ovyo ili waendane na muundo wao,” alisema.

Alisema hatua waliyofikia Simba kimataifa ni nzuri, lakini wanahitaji pia kuwekeza kwa wachezaji ambao watakuwa na Simba kwenye mashindano ya kimataifa si chini ya mara nne.

“Kikosi cha Simba wengi umri umesogea, miaka miwili ijayo bila shaka hawatakuwapo nao, hivyo kuna haja ya kuwekeza kwa wachezaji vijana wazawa ambao watashiriki mashindano ya kimataifa misimu mminne, na ule wa tano, lazima wafanye kitu sababu watakuwa wameiva kiushindani,” alisema.

MKONGO AKOMAA

Kocha Zahera, kwa upande wake amesisitiza kuwa atakomaliza mechi zao sita za mwisho ili kuona msimu huu anaumaliza vipi, lakini akili yake ni kuona wanarejesha taji la Ligi Kuu na kukata tiketi ya CAF kwa msimu ujao wa mashindano ya kimataifa.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Zahera alisema ni ngumu kukata tamaa kwa sasa wakati Yanga inaongoza msimamo na kudai atakomaa na Simba ya kina Kagere sambamba na Azam ili kuona msimu unamalizika kibabe na kubeba mataji ya Ligi Kuu na Kombe la FA ili waende Caf msimu ujao.

“Simba imeshinda zaidi ya michezo 13 mfululizo hakuna ambaye alitegemea kama inaweza kufungwa sasa kakubali kipigo cha bao 2-1 dhidi ya Kagera imepunguzwa pointi, bado ina michezo mingine ya viporo kama kafungwa na hilo linawekezana basi sisi tuna nafasi ya ubingwa, hatukati tamaa,” alisema.

Alisema mbali na kuikomalia Simba, pia wanaipigia hesabu Azam kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo wao na kama watabahatika kukutana kwenye fainali ya FA iwapo kila moja itavuka kikwazo cha nusu fainali basi watakomaa kuhakikisha wanabeba ubingwa huo kwa msimu huu.

“Nawaheshimu Azam wana timu nzuri, ndiyo maana wapo nafasi nzuri katika msimamo wana kikosi kizuri na wao wanapambana kuhakikisha wanasalia nafasi ya pili, nami nahitaji ubingwa pointi zao kwenye ligi zitasaidia kuendelea kujiimarisha kileleni pia kama nitakutana nao FA pambano litaamua wa kuibeba tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika.”

Yanga na Azam zitakutana Jumatatu ijayo katika mechi ya Ligi Kuu Bara likiwa pambano lao la kwanza msimu huu, huku Jangwani wakiwa na kumbukumbu ya kufumuliwa kwenye mechi yao ya mwisho ya msimu uliopita walipotandikwa mabao 3-1.

Yanga haina rekodi nzuri dhidi ya Azam, lakini matumaini yameongezeka kwa Zahera.