Zahera amshtukia beki wake

Monday April 15 2019

 

By Charity James

YANGA wanaelekea mjini Morogoro kwa ajili ya pambano lao la Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, lakini huku nyuma buana, Kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera amemshtukia beki wake mkongwe na fasta kampa kazi ya kufanya ili athibitishe kama anastahili nafasi kwenye mechi zilizosalia.

Si mnajua, hivi karibuni Zahera aliamua kumtumia Juma Abdul katika mechi zake kadhaa baada ya Paul Godfrey ‘Boxer’, lakini sasa unaambiwa Mkongo huyo ameamua kumchunia beki na nahodha huyo wa timu hiyo na kumpa kibarua cha kupunguza uzito mkubwa alionao.

Kocha Zahera amesema kuwa, ili Abdul aweze kumbadili Boxer ni lazima apunguze uzito alionao ili awe fiti zaidi licha ya kukiri beki huyo bado ni mmoja wa mabeki bora wa pembeni aliowahi kuwaona.

Beki huyo alikuwa tegemeo katika kikosi cha Yanga kutokana na uwezo wake wa mkubwa wa kupanda mbele kusaidia mashambulizi, kupiga krosi zenye macho na kushuka kuzuia wapinzani, lakini chini ya Zahera imekuwa tofauti na hivi karibuni wakati Boxer akiwa majeruhi alipewa nafasi na kufanya mambo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera alisema Abdul ni beki mzuri na ana kasi, lakini kama atapunguza kilo alizonazo, lazima atakuwa fiti zaidi na pengine anaweza kupata nafasi kikosini, ila kwa sasa hawezi kumzungumzia kama anaweza kumng’oa Boxer mwenye uwezo mzuri wa kupanda na kushuka.

“Nimemuangalia Abdul katika mchezo wetu dhidi ya African Lyon, anajua sana mpira na ana uzoefu na ligi tunayoishiriki, lakini kinachomuangusha ni mwili mkubwa unaomfanya ashindwe kuwa na kasi ya kuwakimbiza wapinzani hasa upande anaocheza ambao ni muhimu kutengeneza mashambulizi,” alisema na kuongeza;

“Nimekaa naye nimempa programu maalumu ili aweze kudumu katika nafasi hiyo kama alivyokuwa awali, ni lazima apunguze kilo alizonazo sambamba na kufanya mazoezi ambayo yatamsaidia kuongeza pumzi itakayomfanya aweze kupanda na kushuka kama ilivyo kwa Boxer ambaye ana shida moja ya kushindwa kutoa pasi za mwisho kwa usahihi.”

Mkongo huyo aliyeiongoza Yanga kucheza mechi 31 za Ligi Kuu na kushinda 23 kutoka sare tano na kupoteza tatu ikivuna alama 74, alisema endapo Abdul atamudu kufanya alichomuelekeza basi atakuwa na kazi nyingine ya kufanya kuhakikisha anawapanga wachezaji wote wawili katika kikosi kimoja huku akiweka wazi kuwa Boxer anaweza akarudi katika nafasi yake ya winga ambayo mashabiki naamini hawajawahi kumuona akicheza.

KUWATUMIA WOTE

Zahera aliongeza anatamani kila nafasi iwe na wachezaji zaidi ya wawili na wote wawe na uwezo wa kucheza ili wapeane changamoto ya kufanya vizuri na kuisaidia timu kupata matokeo na kuongeza kuwa ana changamoto kubwa katika nafasi ya beki wa kati.

“Unajua mpira ili uwe mzuri na wachezaji wawe na kiwango kizuri,” alisema.

Advertisement