Zahera amshtukia beki wa Kichuya

Muktasari:

  • Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amemwangalia mchezaji wake, Paul Godfrey 'Boxer' na kusisitiza kama atacheza kwa kujituma na umakini, atafika mbali kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha ndani ya kipindi kifupi tangu alipompa majukumu ya kucheza kikosi cha kwanza.

YANGA usiku wa jana walikuwa Uwanja wa Taifa kumalizana na Mbao FC, huku Kocha Mkuu wake, Mwinyi Zahera akiwa kwao DR Congo kwenye majukumu ya kimataifa katika timu yao ya taifa, hata hivyo kabla ya kutimka alishtukia jambo na kulitolea tamko.

Kocha huyo alisema amemwangalia kwa umakini beki wake wa kulia, chipukizi Paul Godfrey ‘Boxer’ kisha kufichua siri moja kubwa kama ataendelea kujituma atakuwa hatari zaidi kufuatia anaweza kucheza nafasi mbili uwanjani.

Zahera alisema Godfrey aliyepewa jina la Boxer akifananishwa na pikipiki yenye jina hilo inayosifika kwa kasi, ni chipukizi mzuri ambaye kama ataendelea na kiwango hicho atakuwa na umuhimu mkubwa katika timu yao.

“Boxer ni kijana mzuri anayejua kusikiliza nini kocha anataka afanye uwanjani, kwanza watu wanatakiwa kuelewa yule sio beki nafasi yake halisi ni winga wa kulia,” alisema Zahera na kuongeza;

“Niliamua kumbadili nafasi baada ya kuumia kwa Juma Abdul lakini kama ataendelea kucheza kwa kiwango bora zaidi katika timu yangu atacheza sana napenda nguvu zake na kasi.”

Zahera alisema bado anaamini chiupukizi huyo aliyefanikiwa kumdhibiti vyema winga Shiza Kichuya wa Simba katika pambano la watani hadi kutolewa uwanjani na Kocha wake, Patrick Aussems, anaweza kufanya vizuri zaidi kwa sababu ya kuwa winga.

Alisema, anaamini baada ya muda mfupi beki huyo atakuwa kwenye anga za mabeki wengine wa kulia wanaotamba ndani na nje ya nchi kama ilivyo kwa Hassan Kessy.

Beki huyo aliyekuwa timu ya vijana ya Yanga, amejizolea umaarufu ghafla kwa soka lake la kasi akizalisha mashambulizi, ingawa bado anaangushwa na uzoefu mdogo alionao, japo katika pambano la watani alikamua vilivyo kama mzoefu vile.