Zahera ampa mzuka kipa Pamba, aipania Ligi Daraja la Kwanza

Muktasari:

Kameni alisema sifa hizo zimempa nguvu katika safari yao ya kuipa mafanikio Pamba kwenye ligi hiyo inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii.

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera amesifu kiwango kizuri cha kipa wa Pamba FC, Idrissa Ramadhani ‘Kameni’ lakini kipa huyo amesema sifa hizo zimempa nguvu ya kupambana kuhakikisha anafanya vyema Ligi Daraja la Kwanza.

Kipa huyo katika mchezo wao na Yanga alicheza vizuri kwa kuokoa mashambulizi jambo lililofanya baada ya mchezo kumalizika kusifiwa na Zahera kuwa alikuwa shujaa kwa timu yake.

Katika mchezo huo wa kujipima nguvu uliopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita Uwanja wa CCM Kirumba, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Kameni alisema sifa hizo zimempa nguvu katika safari yao ya kuipa mafanikio Pamba kwenye ligi hiyo inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii.

“Ukiona umesifiwa na kocha mkubwa kama Zahera ujue kuna kitu umekifanya kizuri, hizi pongeni nitazitumia kama morali ya kuendelea kujituma kuanzia mechi hadi mazoezini,” alisema.

Alisema kwa sasa wanajiandaa kucheza na mechi ya kwanza na Stand United itakaopigwa Septemba 16 uwanja wa Nyamagana ambao ni muhimu kwao kushinda.

“Sasa tuko katika maandalizi ya ligi kwangu mazoezi ninayofanya ni kucheza krosi na mipira ya adhabu kwani nimejikita huko kwa sababu nataka niwe fiti zaidi,” alisema kipa huyo.