Zahera amfunguka ishu ya Banka

Muktasari:

Mkongomani alisema Banka ni kiungo hodari ambapo akili yake, uchezaji na kumudu kucheza nafasi zaidi ya mbili ni vitu anavyovikosa sasa.

KIUNGO mpya wa Yanga, Mohamed Issa 'Banka' bado anaendelea kukosekana katika kikosi chake lakini kocha wake Mwinyi Zahera, amefunguka anachokikosa kwa kiungo huyo kwenye kikosi chake.
Akizungumza na Mwanaspoti jana, Zahera alisema kuendelea kumkosa Banka ni pigo kubwa kwa kuwa kuna kitu kinapungua katika kukamilisha mipango yake kwenye timu hiyo.
Alisema wakati Banka anasajiliwa alikuwa tayari ameshamuweka katika mipango yake kutokana na ubora alioanao, lakini sasa analazimika kutumia mbinu mbadala kukabiliana na pengo lake.
"Siwezi kufurahi kumkosa Banka ni mtu niliyekuwa namuhitaji sana hapa Yannga wakati anasajiliwa nilijua kwa aina yake ni wapi nitamtumia," alisema Zahera.
"Unajua Banka anaweza kucheza nafasi nyingi,anacheza kwa juhudi sana pia ana akili sana hayo ni mambo ambayo nayakosa sasa kwa kuendelea kumkosa."