Zahera ajenga ukuta mpya Mali, Guinea

Muktasari:

Taarifa ambazo Mwanaspoti limepenyezewa, Yanga inasaka beki mmoja wa kati atakayekuja kucheza sambamba na mkongwe Kelvin Yondani, ambaye kwa sasa amekuwa na kiwango bora.


YANGA imepanga kusajili vifaa vinavyotoka nchi zinazozungumza Lugha ya Kifaransa na imefahamika, hesabu zao tayari zipo nchini Mali wakifuata mabeki wawili nchini humo.

Taarifa kutoka ndani ya mabosi wa Yanga, chini ya Kocha Mwinyi Zahera klabu hiyo inapiga hesabu kwa mastaa wa nchi hizo kwa sababu sio wasumbufu na tayari mchakato umeanza.

Taarifa ambazo Mwanaspoti limepenyezewa, Yanga inasaka beki mmoja wa kati atakayekuja kucheza sambamba na mkongwe Kelvin Yondani, ambaye kwa sasa amekuwa na kiwango bora.

Hesabu za Yanga ni kutua nchini Guinea ikiwafuata mabeki wawili katika klabu moja iliyoshiriki michuano ya Caf mara tatu mfululizo.

Jicho la Yanga lipo katika klabu ya Horoya ambayo msimu huu imeishia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambako jicho lao limetua kwa beki mmoja wa kazi.

Ingawa Yanga wamekuwa wazito kutoa majina ya vifaa hivyo, lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa tayari mazungumzo kunasa huduma za mabeki Boubacar Samassekou, raia wa Guinea na Hamed Assoko raia wa Mali.

Uimara wa mabeki hao umeifanya Horoya kufika hatua hiyo ya ligi ya mabingwa na wamekuwa na kazi nzuri ya kulinda lango lao.

Utamu wa Assoko ni msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika hadi chama lake linatolewa, alikuwa ametupia nyavuni mabao mawili na ni mtaalamu wa kupandisha mashambulizi

Kama Yanga itamnasa mmoja kati ya Samassekou au Assoko kisha kuunganishwa na Yondani kujenga ukuta wa Yanga, msimu ujao mastraika kama Emmanuel Okwi, Meddie Kagere watakuwa na kazi ya ziada kuipenya ngome ya Yanga.