Zahera afyatuka ratiba mbovu Ligi Kuu

Muktasari:

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera ameishauri TFF kupanga ratiba yenye faida ikiwemo kuweka mechi za usiku kwa siku za katikati ya wiki na  mechi za jioni kwa siku za mwishoni mwa wiki.

Dar es Salaam.Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera amesema upangaji mbovu wa ratiba naaamuzi mabovu ya waamuzi yanarudisha nyuma Soka la Tanzania.
Zahera  alisema haiwezekana timu nyingine ziwe zimecheza mechi mfulizo na nyingine zikiwa na viporo kwani hiyo inapunguza ushindani wa ligi.
Anashangaa kuona Simba imerudi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku ikiwa  haina mechi yoyote ya Ligi inayopaswa kucheza wiki hii.
"Inashangaza jinsi ratiba inavyopangwa kwani wakati tunashiriki Kombe la Shirikisho Afrika tunatoka mfano Rwanda tunarudi tunaenda shinyanga kucheza mechi ya ligi halafu tena Rwanda halafu tunarudi kucheza mechi nyingine ya ligi
"Lakini Simba inacheza mechi za kimataifa na  imerudi lakini inapumzika  wiki nzima bila  mechi ya Ligi, inashangaza kwani mpira hauwezi kuendelea hivyo "alisema Zahera.
Zahera alisema yeye hupenda kuongea ukweli na haogopi timu anazokutana nazo kwenye ligi anawaogopa watu wanaochangia kurudisha nyuma maendeleo ya Soka.
"Mpira hauwezi kupanda  kama kuna watu wanakuja na lengo la timu fulani ibebe Kombe.
"Sidhani Kama TFF inawatuma waamuzi kufanya hicho wanachokifanya uwanjani bali kuna watu  wanaingilia na kuchafua mpira wa Tanzania.
"Kama TFF wanataka mpira uendelee fungia miaka 10 waamuzi wa namna hiyo kwa sababu wanaitia aibu nchi kwani ligi inaonyeshwa nchi mbalimbali na watu wanaona na kushangaa maamuzi mabovu wanayotoa waamuzi" alisema Zahera.