Zahera afichua ishu ya Makambo kuuzwa Sh200 milioni

Muktasari:

Makambo alisaini mkataba huo chini ya Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera mkataba unaodaiwa kuwa na thamani ya Dola 100,000 zaidi ya Sh 200 milioni.

STRAIKA wa Yanga, Haritier Makambo wiki hii ameelezwa kusaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia timu ya Horoya AC ya Guinea huku usajili wake ukizua mjadala mkubwa kwamba, amesajiliwa kinyume na makubaliano kwa kuwa ana mkataba wa zaidi ya mwaka mmoja na Yanga.

Makambo alisaini mkataba huo chini ya Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera mkataba unaodaiwa kuwa na thamani ya Dola 100,000 zaidi ya Sh 200 milioni.

Baada ya usajili huo, kulitokea mgongano kuwa mchezaji huyo alikuwa akiichezea Yanga kwa mkopo akitokea FC Lupopo ya DR Congo, jambo ambalo Zahera ameweka wazi kwamba Makambo ni mali halali ya Yanga.

Makambo alitua Yanga kwa mkataba wa miaka miwili ambao, unamalizika msimu ujao hivyo kuondoka kwake kutawapa Yanga mamilioni ya fedha kwa kuvunja mkataba wake.

Hata hivyo, Zahera jana Jumamosi baada ya kutua nchini aliruka kihunzi kwa kusema hawajamalizana na Horoya hivyo, haujakamilika mpaka sasa.

“Bado hawajamalizana, hiyo sio ya kweli mpaka pale ambapo, nitasema mambo yapo kwenye mazungumzo. Tulikwenda kuzungumza nao na sio kwamba kumalizana, hivyo kusafiri sio kumaliza mambo ndiyo maana nasema mazungumzo yanaendelea.

“Makambo ni mchezaji wa Yanga na ligi inaendelea, ikimalizika kila mtu atajua anakwenda wapi, hata akiondoka tutapata mchezaji mwingine mzuri zaidi yake na kuifanya Yanga kuwa moto zaidi.

“Makambo akiuzwa pesa yote itachukuliwa na Yanga, wakati anatoka DR Congo alikuwa na timu yake na haikuwa mkopo, Makambo sio mchezaji wangu ana wakala wake ila aliniomba tu nimsaidie ili asidanganywe hata wakala wake aliniomba niende nikamsaidie kwa sababu nafahamu mambo mengi.

“Nawaambia Wanayanga wajue kwamba, kama Makambo anauzwa wataambiwa kama atabaki pia watajua kwani, huko anakotaka kwenda mshahara ni mzuri pengine kuliko hata hapa, hivyo akienda itamsaidia. Soka ni kazi na Yanga haiwezi kuzuia mchezaji kama anakwenda mahali ambakowatanunua mkataba wake na kumlipa vizuri, mchezaji ataamua.

“Makambo ni mchezaji anayeombwa kwenda huko na wakikubaliana basi hakuna tatizo ataondoka,” alisema Zahera alipohojiwa na kituo na Wapo Radio