Zahera: Tulieni muone mambo

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera alisema maandalizi ya mechi tatu zilizopita alizoambulia pointi tano viongozi hawakuzungumzia michezo hiyo zaidi ya kukumbusha tu kuwa kuna mechi mbele yao dhidi ya watani, kuonyesha walivyo na presha kubwa kuelekea mchezo huo.

MABOSI wa Yanga pamoja na wanachama na mashabiki presha zimeanza kuelekea kwenye pambano lao la watani zao wa jadi, Simba watakaocheza nao Jumamosi hii, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera amedai kushangazwa na presha hizo na kuwatuliza kimtindo.

Kocha Zahera amesema ameshangazwa na presha ya viongozi wake kuelekea mchezo huo na kuweka wazi kama mzuka huu ungekuwa kwenye michezo yote, basi wangetangaza ubingwa mapema.

Vigogo hao wa soka watavaana katika pambano lao la 102 tangu Ligi Kuu ianzishwe mwaka 1965 huku kila moja ikisaka ushindi kwa vile mchezo wao wa kwanza uliopigwa Sept 30, 2018 ambao Simba ilikuwa mwenyeji matokeo yalikuwa suluhu (0-0).

Tangu ifahamike kuwa pambano hilo litapigwa Feb 16, upande wa Jangwani presha imekuwa kubwa, kulinganisha na watani zao ambao leo watakuwa kwenye majukumu ya kimataifa dhidi ya Al Ahly, lakini Kocha Zahera amewataka Wanayanga kutulia kwani yajayo Jangwani yanafurahisha, huku akisisitiza maandalizi yake ni kama ya mechi nyingine kwani haoni tofauti.

Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera alisema maandalizi ya mechi tatu zilizopita alizoambulia pointi tano viongozi hawakuzungumzia michezo hiyo zaidi ya kukumbusha tu kuwa kuna mechi mbele yao dhidi ya watani, kuonyesha walivyo na presha kubwa kuelekea mchezo huo.

“Nimegundua timu inaendeshwa kwa presha ya ‘derby’, haya mambo hayapo Tanzania tu nchi zote kuna timu ambazo zikikutana mechi yao inavuta hisia za mashabiki, lakini hawana presha kama ilivyo hapa Tanzania hadi viongozi wanashindwa kufanya kazi kwa kuhangaikia mchezo mmoja ambao pia unazalisha pointi tatu,”

“Ni jambo la kushangaza na kusikitisha upande wangu naamini michezo yote hata nikishinda dhidi ya Simba siwezi kukabidhiwa taji siku hiyo hadi nitakapomaliza kucheza mechi zote na timu zinazoshiriki Ligi Kuu, kwanini niamini kumfunga mpinzani wangu ni kumaliza kila kitu?”

Lakini alisema licha ya presha hizo zote za mabosi na hata mashabiki na wanachama kwa upande wake maandalizi ya kuelekea mchezo huo kwa timu yake yatakuwa ni ya kawaida tu kama wanavyofanya wanapokutana na timu nyingine.

Zahera alisema anaamini ushindi wake dhidi ya JKT Tanzania Juzi Jumapili umeongeza molari kwa nyota wake kuendelea kupambana zaidi, hivyo hata Jumamosi mambo yanaweza kuwa mazuri kwao japo anakiri huenda pambano hilo likawa gumu kwa ushindani uliopo baina ya timu hizo.

Kocha huyo aliyeiongoza Yanga katika mechi 23 na kushinda 18, kupoteza mchezo mmoja na kutoka sare michezo minne na kukusanya jumla ya alama 58, alisema kila mchezo uliobaki mbele yake anauchukulia kwa upana zaidi tofauti na viongozi wake ambao wanaupa kipaumbele zaidi mchezo dhidi ya Simba na kuwaomba kufanya maandalizi mazuri ili kutimiza lengo lake la kupata pointi tatu kwa kila mechi.

Aliongeza kikubwa anachoweza kukizungumzia kwa sasa ni ratiba ngumu kwake na angependa kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi, mashabiki na timu kwa ujumla kuwa pamoja na kucheza kwa kujituma ili kuweza kupata ushindi kwa kila mchezo ili kutimiza malengo yao.