ZUCHU: Nataka mume wa aina hii

Jana Jumapili tulianza na makala ya nyota mpya wa kike kutoka lebo ya WCB, Zuchu ambaye alianika mambo yake kadhaa ikiwamo kuruka kimanga kuwa na uhusiano na bosi wake na staa wa muziki wa kizazi kipya nchini anayemiliki lebo hiyo, Diamond Platnumz.

Pia Zuchu aliweka bayana kuwa na tatizo la pumu ambayo imemfanya awe anatembea na dawa kwenye mkoba wake, ili likitokea la kutokea aweze kuweka mambo sawa mapema na kueleza namna tuzo za Afrimma zilivyompagawisha kwa kuteuliwa kuwania mwaka huu.

Leo mwanadada huyo, aliye mtoto wa Malkia wa Mipasho nchini, Khadija Kopa anamaliza mfululizo wa makala haya yaliyotokana na mahojiano maalum aliyofanyiwa nyumbani kwa Diamond na anaweza bayana aina ya mwanaume anayemtaka we mumewe. Endelea naye...!

MKWANJA WA JOKETI

Katika kufunguliwa milango ya kulipwa kwenye shoo, Zuchu anasema wa kwanza kumlipa alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo alipompatia mwaliko wa kwenda wilayani humo kwenye uzinduzi wa mradi wa maji.

Hata hivyo, pesa hiyo anasema hakuna cha maana alichoifanyia zaidi ya kununua vitu vyake vya usichana lakini sio kitu ambacho cha kukaa na kukumbuka hiki nilinunua kwa fedha hizo.

MUME AMTAKAYE

Kama walivyo wasichana wengine hapo baadaye kutaka kuolewa, Zuchu ambaye anaeleza kwa sasa yupo singo, anasema mwanaume anayetamani aje kuwa mumewe ni mtu asiyejihusisha na masuala ya sanaa.

Anasema anaamini akiwa hivyo atakuwa na uwanja mpana wa kujifunza kazi ingine nje ya sanaa kuliko kufanya kazi zinazofanana.

Wakati kuhusu suala la watoto anasema angependa azae watoto wawili na ikiwezekana mapacha.

Alipoulizwa juu ya kuolewa mitala, kutokana na kuonekana kuwa fasheni kwa wasanii wenzake wanaofanya kazi WCB naye anasema hawezi kutoa jibu la moja kwa moja kwa kuwa hajui Mungu amempangia nini.

“Kwa kweli tusubirie tu, kwani hata hiyo ndoa ya mitala leo unaweza kuikataa baadaye ukajikuta unakuja kuwa singo maisha yako yote, tuliache kwanza hilo kwani kesho aijuae ni Mungu pekee.”

AMTAMANI NANDY

Wakati watu wakimpambanisha na Nandy katika muziki kwa sasa, Zuchu anasema ni mkali huyo ni mtu anayemkubali na kumheshimu sambamba na kupenda juhudi zake anazozifanya katika kuusukuma muziki wake.

Ni kutokana na kuvutiwa huko anasema anatamani siku moja kufanya kolabo na msanii huyo kama menejimenti zao zitakubaliana kwani anaamini kipaji alichonacho tangu walivyokutana kwenye mashindano ya Tecno On The Stage nchini Nigeria.

HARMONIZE, RAYVANNY WAHUSIKA

Zuchu anafichua kukutana kwake na Diamond kwa siku ya kwanza membaz na makaka zake ndani ya Lebo ya WCB, Rayvanny na Harmonize wanahusika.

Anasema anakumbuka siku ya kwanza kukutana na Diamond ilikuwa siku mama yake (Khadija Kopa) ameandaa shoo mkoani Morogoro na kutaka kwenda kuwakodi Rayvanny na Harmonize.

Katika safari hiyo alimuomba mama yake waongozane na Malkia wa Mipasho wala hakusita kwenda naye na alimkubalia kwa kumwambia huenda akapata wasaa wa kuonana na Diamond.

“Kweli bwana, kama zali siku hiyo kama bahati mama anafika ofisi za WCB wakati huo zikiwa maeneo ya Sinza na kumuona Diamond, ambapo alimuelezea nia yangu ya kutaka kuingia kwenye muziki,” anasema Zuchu na kuongeza;

“Ndio hapo aliponipa masharti nitatakiwa kufanya usaili ili kunipima uwezo wangu katika kuimba na nishakuru jambo hilo limekamilika na leo nipo WCB. Kama sio kutaka kuwakodi kina Harmonize na Rayvanny huenda nisingetua katika lebo hii.”

RATIBA YAKE

Kuhusu ratiba yake ya kila siku, Zuchu anasema huwa haitabiriki, kwani kuna wakati humbana na hasa anapokuwa na kazi studio.

“Huwezi kuamini kuna wakati huwa natoka nyumbani kwa Diamond saa 9 usiku ama saa 11 alfajiri kwa kazi za kurekodi, lakini nikiwa nipo frii huwa ni ya kawaida kama ilivyo kwa wasichana ama wasanii wengine wanaojitambua,” anasema Zuchu na kudokeza, licha ya muziki, lakini kitaaluma yeye amesomea masuala ya biashara na uchumi, anasema ndoto zake kwenye maisha mbali na muzik anapenda kuwa mfanyabiasha.

Anasema licha ya kuingia kwenye muziki anjua kwamba hiyo ni moja ya njia ya kufanikiwa katika biashara na kueleza kuwa kingine kinachomsukuma huko ni kutokana na nchi ya Tanzania kuwa na vitu vingi kama fursa ya kufanya biashara.

“Mbali na Tanzania kujaliwa rasilimali nyingi za kutwezesha kufanya biashara pia kusoma kwangu India kumenifungua macho katika vitu vingi sana, kule hakuna fursa wanayoiacha iwapite hivihivi kila kitu wakionacho mbele yao wao wanawaza kuifanyia biashara.

JIDE, RAY C

WAMBADILISHA UPEPO

Zuchu anakiri licha ya kwamba mama yake na baadhi ya ndugu zake wanaimba muziki wa taarabu, lakini alijikuta akibadilisha upepo na kuingia kwenye Bongofleva kwa sababu ya kina Lady Jaydee na Ray C alioanza kuwasikia kitambo na kuwafuatilia kila hatua walizopiga kimuziki.

“Nilitamani kuja kuwa kama wakali hao wawili sambamba na Vanessa Mdee na ninashukuru hayo yameanza kuonekana ikiwemo kukutana ana kwa ana na Jide.”