ZFA wasotea udhamini wa ligi

Muktasari:

Kuna baadhi ya kampuni zimefuatwa moja kwa moja na na viongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na nyingine zimefuatwa na wadau wa soka wenye kupenda maendeleo ya mchezo huo visiwani humo.

LIGI Kuu Zanzibar imeingia mzunguko wa pili ikiwa ni mechi ya 22 kwa timu shiriki huku hali ya uchumi ikiendelea kuitesa ligi hiyo baada ya Kamati ya Mashindano kutamka haijapata mdhamini hadi sasa.

Kamati hiyo ilisema licha ya kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha ligi hiyo inakuwa na wadhamini lakini jitihada zao hazijazaa matunda.

Akizungumza na gazeti hili, katibu wa kamati hiyo, Alawi Haidar Foum alisema bado wanaendelea kufanya mazungumzo na baadhi ya makampuni ndani na nje ya Zanzibar.

Alisema kuna baadhi ya kampuni zimefuatwa moja kwa moja na na viongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na nyingine zimefuatwa na wadau wa soka wenye kupenda maendeleo ya mchezo huo visiwani humo.

Alawi aliwatoa hofu mashabiki wa soka Zanzibar kwa kusema kamati hiyo ipo makini kuhangaika kuona mpira unabadilika kwa maeneo yote kwa kuzipunguzia timu gharama za uendeshaji.

Alisema licha kutopata udhamini, kamati hiyo itahakikisha inasimamia nidhamu viwanjani kwa kuzichukulia hatua timu zitakazovunja kanuni.