Yule Chief wa Kauzu FC aitaka Taifa Stars sasa!

Thursday September 13 2018

 

By Charity James

Dar es Salaam. Shabiki maarufu wa Kauzu FC, Juma Ally 'chief' amesema anatamani kuwahamasisha wachezaji wa Taifa Stars katika ushangiliaji kinachomtia ukakasi ni viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutompa ushirikiano.

Chief amesema,  ametumia nafasi hii kuiomba TFF kumpa nafasi ili aweze kufanya  kazi na kuwahamasisha mashabiki, wajitokeze kwa wingi kuipa ushirikiano Taifa Stars kama wachezaji wa 12 uwanjani.

"Kama kutakuwa na mtu yeyote ambaye anaweza kunipa ushirikiano akaniita tukakaa meza moja na kuzungumza kuhusiana na kutafuta kikundi cha ushangiliaji, mimi binafsi nitafanya kazi ya kuwashawishi watu ili waishangilie Taifa Stars,"alisema Chief.

Chief amesema anaipenda nchi yake na timu yake ya taifa ambayo ina wachezaji zaidi ya wanane nje ya Tanzania na imeanza kwa kasi michuano ya kuwania kufuzu fainali za AFCON kwa kutoa suluhu na Uganda 'The Cranes'.

"TFF wajue kuwa sisi tupo na wanachotakiwa ni kututumia vizuri ili Taifa Stars iweze kufanikiwa, binafsi naweza kuwaunganisha mashabiki kutoka Arusha, Mwanza, Singida na Mtwara wanaweza wakaja kuishuhudia timu yao ikicheza kutokana na ushawishi wetu," alisema Chief ambaye umaarufu wake umetokana na michuano ya Ndondo.

Advertisement