Yondani azua utata Namungo

USAJILI wa nyota wawili wapya wa Namungo, Kelvin Yondani na Adam Salamba umezua utata, huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likikacha kutoa ufafanuzi kanuni zipi zilizotumika.

Namungo imetangaza kuwaongeza Salamba na Yondani aliyetemwa na Yanga hivi karibuni, huku dirisha la usajili likiwa limeshafungwa tangu Agosti 31 na orodha mpya ikitangazwa kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Septemba 6.

Salamba tayari alicheza mechi ya Namungo walipochapwa 1-0 na Tanzania Prisons, huku Yondani akitangazwa jana na Katibu Mkuu wa timu hiyo, Ally Seleman kwa mkataba wa mwaka mmoja.

“Tumemsajili Yondani kwa mkataba wa mwaka mmoja kama mambo yatakuwa vizuri tuna nafasi ya kumwongeza mwingine ndani yake au utakapomalizika, lengo likiwa ni kwa michuano ya kimataifa,” alisema Seleman.

Hata hivyo, kanuni za soka zinaeleza usajili wa wachezaji hufanyika kipindi cha dirisha tu, licha ya zile za kimataifa kutoa nafasi kwa walio huru kusajiliwa muda wowote, huku Tanzania ikiwa haiitumii katika kanuni zake jambo lililofanya Mwanaspoti kuwatafuta viiongozi wa TFF waliokuwa wakipasiana kutolea ufafanuzi.

Mkurugenzi wa Mashindano, Salum Madadi alisema yupo safarini hivyo asingeweza kutoa ufafanuzi, huku Mwanasheria wa TFF, Herman Kidifu naye alisema;

“Nikilifuatilia ndipo nitakuwa na cha kujibu ya kuelezea juu ya usajili huo.”

Lakini mmoja wa viongozi wa shirikisho hilo aliyeomba kuhifadhiwa jina alisema; “Nadhani ufafanuzi wa usajili wa wachezaji hao utatolewa, japo hakuna kanuni inayoruhusu kusajili baada ya dirisha la usajili kufungwa.”

“Kinachofanyika, kama mchezaji ni huru na maelezo yaliyotolewa na timu yana tija, wanaangalia namna ya kusaidia na kumwingiza katika usajili, hiyo ni pamoja na kuangalia namna ya kulinda kipaji chake. Ingawa kuna wale majina yao yanasahaurika kuingizwa kwenye TMS ila napo hayaingizwi baada ya majina kutangazwa, hivyo wahusika watalitolea ufafanuzi madamu walitangaza usajili mzima,” alisisitiza kiongozi huyo.