Yondani afichua siri miaka 13 Simba, Yanga

Muktasari:

Alisema anapokuwa uwanjani anapenda kuzingatia kile ambacho kimemfanya awe uwanjani hao na anajituma kwa bidii na mizaha yote anaiweka pembeni.

KAMA hujui huu ni msimu wa 15 tangu beki mkongwe nchini Kelvin Yondani awe katika Ligi Kuu akizichezea Simba na Yanga sambamba na Taifa Stars tena akiwa na utamu ule ule.

Jambo hili limekuwa likistaajabisha mashabiki wengi wa soka, lakini mwenyewe buana amefichua siri ya kucheza kwa kiwango cha juu kwa muda wote wa miaka 13 tangu atue klabu za Kariakoo.

Yondani ameichezea Simba kwa misimu saba mfululizo, kuanzia mwaka 2006-2012 kabla ya kuhamia Yanga anakokipiga mpaka sasa ukiwa ni msimu wake wa nane.

Katika misimu yote 15 aliyozichezea timu hizo, beki huyo amekosa mpinzani na akinyakua jumla ya mataji sita ya Ligi Kuu ndani ya misimu hiyo akiwa ndiye mchezaji pekee wa klabu hizo mbili kubeba mataji mengi kwa wachezaji wanaozichezea kwa sasa.

Beki huyo wa kazi, ambaye mwonekano wake tu unatuma salamu kwa washambuliaji sio mtu wa mzaha awapo kazima amefichua sababu ya kiwango chake kutoshuka, licha ya kucheza mfululizo kwa miaka yote katika Ligi Kuu, akidai ni mambo matatu tu yanayombeba.

Aliyataja mambo hayo ni kujituma mazoezini, kuliheshimu soka kama sehemu inayomwingiza riziki zake za kila siku na kuutunza mwili wake kila uchao.

Alisema anapokuwa uwanjani anapenda kuzingatia kile ambacho kimemfanya awe uwanjani hao na anajituma kwa bidii na mizaha yote anaiweka pembeni.

“Kwanza napenda kufanya mazoezi, yale ya timu na yangu binafsi, ili nikiingia kucheza nifanye kile ambacho ndio lengo la kocha kulipata kwangu, kifupi dakika 90 huwa sina masihara hata kidogo,” alisema Yondani ambaye si mwongeaji sana kwenye vyombo vya habari.

“Laiti kama roho ninayokuwa nayo uwanjani ndio ningekuwa naishi nayo nje ya kazi basi ningekuwa nimefungwa, lakini nje ya kazi mimi ni mpole nisiyetaka makuu wala mambo mengi,” aliongeza beki huyo anayeicheza pia Taifa Stars.

Alipoulizwa pamoja na ustaa alionao si mtu anayependa kujionyesha kwa watu ni kitu gani kinafanya aishi maisha hayo? Alianza kwa kutabasamu kisha alisema; “Nikimaliza kazi yangu uwanjani sina muda wa kushoo vitu huwa naendelea na maisha yangu. Napenda kazi yangu ndio maana naitendea haki, bila kujitunza, kujua unachofanya kwenye soka ni ngumu kudumu kwenye kiwango, hilo ndilo naweza kulisema.”

Mbali na kucheza kwa bidii, pia Yondani ni kati ya mabeki ambao wamekuwa wakifunga mabao, wakati mwingine kwa mikwaju ya penalti, ingawa kuna muda hushindwa kuhimili mizuka ya soka uwanjani na kufanya mambo yanayogharimu timu ikiwamo kupewa kadi nyekundu.

Moja ya tukio linalokumbukwa ni kitendo chake cha kumtemea mate aliyekuwa beki wa Simba, Asante Kwasi katika mechi yao ya watani iliyopigwa Aprili 29, 2018 na Yanga kulala kwa bao 1-0 lililofungwa na Erasto Nyoni kwa kichwa katika dakika ya 37.

MAKOCHA WAMZUNGUMZIA

Baadhi ya makocha wamemzungumzia beki huyo, akiwamo Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ aliyesema kiufundi anachokifanya Yondani uwanjani kinatokana na mazoezi anayoyafanya yanayomuweka kuwa fiti.

Pamoja na kukubali kiwango chake, alimshauri Yondan kuendana na nyakati zilizopo akimtaka kuachana na utoto wa mjini ili kama hatakwenda kucheza soka la nje basi amalize kwa heshima kama Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

“Kwanza nampongeza ana nidhamu ya soka sana ndio maana kiwango chake hakiyumbi, ila akitaka kumaliza soka hapa hapa Bongo basi ajitahidi kulinda mwisho wake uwe mwema ili heshima yake iendelee kubakia kama alivyofanya Cannavaro kufuata wachezaji wa zamani,”

“Pia aangalie kile kinachofanywa na Juma Kaseja amepambana na kurejesha heshima yake baada ya kurejea kwa kishindo timu ya taifa, kikubwa apunguze utoto wa mjini mwingi, kiuwezo yupo sawa,” alisema Julio.

Aliyekuwa kocha wa Stand United ‘Chama la Wana’, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema Yondani ni mchezaji anayejitambua na anaamini atafika mbali na kuwaacha chipukizi wakepotea.

“Kuna wachezaji wachache wa kizazi hiki watakaostafu na heshima kama ilivyokuwa kwa wachezaji wa zamani mfano Yondani, Erasto Nyoni, Juma Kaseja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kaacha soka kwa heshima kubwa,” alisema.