Yondani: Kwa 150 milioni, Zesco wanapigwa

Muktasari:

Yondani ameliambia Mwanaspoti kujituma na kutambua umuhimu wa nafasi hiyo ndio chachu ya kuweza kufikia mafanikio.

BAADA ya kuivusha Taifa Stars hatua ya makundi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia, beki wa timu hiyo na Yanga, Kelvin Yondan amesema sasa anahamishia nguvu kwenye jukumu kubwa linalowasubiri Septemba 14 ambapo wataikaribisha Zesco ya Zambia.

Yanga itacheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mabingwa hao wa ligi Zambia katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga ipo jijini Mwanza kwa kambi ya maandalizi yao kuelekea mechi hiyo, ambapo imecheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Pamba na kutoka sare ya bao 1-1 huku leo Jumanne itacheza na Toto Africans na kurejea jijini Dar es Salaam kuisubiri Zesco.

Kamati ya Mashindano ya Yanga, ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha wanashinda mechi hiyo huku ikielezwa imetenga kitita cha Sh 150 milioni kwa ajili ya maandalizi.

Yondani ameliambia Mwanaspoti kujituma na kutambua umuhimu wa nafasi hiyo ndio chachu ya kuweza kufikia mafanikio.

Alisema amemaliza jukumu moja ambalo Watanzania waliowengi walitamani kuona namna gani watafanya kazi sasa anageuka upande wa pili wa timu yake kuhakikisha wanafikia lengo la kuiondoa Zesco na kuingia hatua inayofuata.

“Tumemaliza suala la Stars ninachoweza kuzungumza sasa ni kuhusiana na jukumu lingine kubwa ambalo lililopo mbele yangu, natarajia kucheza mchezo wa kimataifa Jumamosi dhidi ya Zesco ni mchezo ambao unatarajiwa kuwa mgumu kwa pande zote mbili kutokana na kila mmoja kutafuta nafasi.

“Tunaanza uwanja wa nyumbani tunatakiwa kutumia faida ili tuweze kuwa na mchezo rahisi ugenini tunawaomba Watanzania waliojitokeza kuisapoti Stars wajitokeze pia Jumamosi kutupa ushirikiano ili tuwafunge wapinzani wetu,” alisema.

Yondani alisema haitakuwa rahisi kwao kupata matokeo kutokana na kikosi chao kutokuwa na muunganiko mzuri baada ya kusajiliwa kwa nyota wengi wapya na kusalia na wachache ambao walicheza msimu uliopita lakini lengo lao ni kupata matokeo kwa mbinu zozote.

“Tunashuka dimbani tukiwa na kumbukumbu ya kuambulia ushindi wa bao moja ugenini katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa hatuna cha kupoteza kwenye uwanja wetu wa nyumbani kikubwa ni sisi kuwa wamoja na kutimiza mipango yetu.

“Nadhani tunacheza na timu ambayo inanolewa na kocha ambaye analifahamu soka letu vizuri japo anakuja kipindi ambacho nyota wake wengi aliowafundisha hawapo kwenye timu, kikubwa anafahamu mbinu nyingi za soka letu tunatakiwa kujipanga kuanzia huko kabla hatujaruhusu kututawala nyumbani,” alisema Yondani.

Naye nahodha wa timu hiyo, Papy Tshishimbi alisema wamewafuatilia wapinzani wao na kubaini wapo vizuri eneo la kiungo, hivyo wanafanyia kazi hilo kabla ya mchezo huo.

“Ni muhimu kuwasoma wapinzani wetu ili tuweze kuingia kwa nidhamu tumepata nafasi ya kuwafuatilia na kugundua safu yao ya kiungo ni bora na hiyo ndio inatengeneza mabao, hivyo mwalimu tayari ameanza kufanyia kazi eneo hilo ili kupunguza makosa,” alisema na kuongeza:

“Ukishamjua mpinzani wako ubora na udhaifu wake ni rahisi kupata matokeo hatuna maana kwamba kufahamu hayo ndio tumemaliza mchezo, hapana tunawaheshimu wapinzani na tunaendelea kujifua lengo ni kuona tunaonyesha ushindani mkali kwa wapinzani hao na kuibuka na ushindi,” alisema.