Yanga yawaponza Sahare

Muktasari:

Ni mchezo wa Daraja la Kwanza kundi B ambao utapigwa uwanja wa Gwambina mjini Misungwi ambapo wenyeji hao wamesema wanataka kupata ushindi ili kupoza machungu ya kichapo cha 1-0 walichokipata kutoka kwa Yanga kwenye mchezo wa kombe la FA.

KILA mbabe ana mbabe wake Gwambina FC imesema hasira zao za kushindwa kufuzu robo fainali ya Kombe la FA baada ya kufungwa na Yanga sasa wanajipanga kuzoa pointi dhidi ya Sahare All Stars mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) utakaopigwa kesho Jumamosi wilayani Misungwi.
Gwambina yenye maskani yake mjini Misungwi mkoani inaongoza kundi lao wakiwa na pointi 31 wakifuatiwa na Geita Gold wenye alama 25 huku tayari wamecheza michezo 15.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo Athumani Bilali ‘Bilo’ amesema ili wawe sawa ni lazima wawafunge Sahare katika mchezo huo wa kundi B kwani bado machungu  ya kipigo cha Yanga hakijawaisha.
“Ili tuweze kuwa sawa ni lazima tupate ushindi kwenye huu mchezo kwani kutolewa kombe la FA na Yanga kumetuvuruga sana hivyo tunatakiwa tuondoe haya mawazo kwa kuwatandika Sahare,” alisema Bilo.
Alisema mchezo huo utakuwa muhimu kwao kupata ushindi kwani utawafanya waendelee kuwa vinara wa kundi hilo hivyo ni lazima wapambane wapate  pointi tatu.
Bilo alisema anajua ugumu wa mchezo huo hivyo wataingia katika pambano kwa umakini mkubwa kwani wapinzani wao ni wazuri hivyo ni lazima wapambane ili kuwafunga.
“Ni pambano ambalo kwetu tunahitaji ushindi unajua kwa sasa tunafukuzana na Geita Gold hivyo ni muhimu kila mchezo tutakaocheza kuhakikisha tunapata pointi tatu ili kuendelea kuongoza kundi”alisema Bilo.