Yanga yavunja mwiko Musoma, Kaze achekelea

MUSOMA. Akili, nguvu na kasi aliyotumia winga wa kulia, Ditram Nchimbi na kazi nzuri aliyoifanya Straika, Michael Sarpong imeiwezesha Yanga kuibuka na pointi tatu muhimu katika mchezo wao dhidi ya Biashara United.

Katika mchezo huo ambao unapigwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini hapa, haikuwa kazi rahisi kwa timu hiyo kuweza kuondoka na alama tatu kutokana na ushindani ulivyokuwa kwa wapinzani hao.

Hesabu nzuri na mbinu alizotumia Kocha Cedrick Kaze kwa mabadiliko alipomtoa Waziri Junior ambaye alionekana kupoteza mipira mingi na kumwingiza Tuisila Kisinda, ilichangamsha mpira na kusababisha matokeo hayo mazuri.

Ilikuwa dakika ya 76 ambapo Nchimbi alipotumia akili kufuata mpira uliokuwa unaelekea nje na kuuondoa kwa pasi nzuri ambayo ilimkuta Sarpong kwa kichwa na kuujaza mpira wavuni.

Bao hilo lilionekana kuwachangamsha Yanga wakiendelea kulisakama lango la wapinzani na dakika ya 86 Sarpong alikosa bao la wazi baada ya kupokea pasi fupi ya Yacouba Songne ndani ya 18 na shuti lake kuishia mikononi mwa Kipa Daniel Mgore.

Hata hivyo katika mechi hiyo, Makocha wa timu zote walifanya mabadiliko, ambapo Yanga iliwatoa Waziri Junior, Ditram Nchimbi (aliyeumia) na Feisal Salum na kuingia Tuisila Kisinda, Yacouba Sogne na Zawadi Mauya.

Biashara United waliwapumzisha Gerard Mathias na Mustha Hamis na nafasi zao kuchukuliwa na Kelvin Friday na Gerishon Samwel, mabadiliko ambayo yaliwapa faida Yanga kwa kuondoka na alama tatu na kwenda nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi 22 nyuma ya Azam kwa tofauti ya magoli.

Kwa matokeo hayo, Yanga chini ya Kocha wake Kaze, inaendelea kuweka rekodi ya kushinda mechi ya nne mfululizo, lakini zaidi ikitoa gundu na kuondoa uteja kwa Biashara United ambao walikuwa wakiwapa wakati mgumu kwenye uwanja wa Karume Musoma ambapo katika mechi mbili za nyuma Yanga imefungwa moja na kutoka suluhu mechi moja.

 

MSIKIE KAZE

Kocha wa Yanga Cedrick Kaze amesema amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wake na kwamba kipindi cha kwanza kulionekana mapungufu ya kushindwa kutumia vyema nafasi walizopata.

Amesema kubwa anashukuru kwa kupata ushindi kwa timu hiyo ambayo kwa rekodi ilikuwa ikiitesa sana Yanga inapokuwa uwanja wake wa nyumbani na kwamba bado kazi inaendelea.

"Leo nafurahi tumepata pointi tatu, haikuwa kazi rahisi kwa sababu wapinzani walionesha ushindani lakini niwapongeze vijana wangu nao walipambana kusaka kitu na hatimaye kuweza kushinda na kuvunja mwiko," amesema Kocha huyo.

Kwa upande wake Kocha wa Biashara United, Francis Baraza amesema vijana wake wamefanya makosa kidogo ambayo yamewapa faida wapinzani na kwamba mchezo haukuwa rahisi kwani kila timu ilijitahidi kusaka ushindi.

Amesema yeye kama Kocha ataenda kurekebisha kasoro zilizoonekana katika kikosi chake na kwamba katika mechi zijazo anaamini watafanya vizuri.

"Tumefanya makosa madogo ambayo yamewapa faida wapinzani, kucheza na timu hizi kubwa hupaswi kuwa na presha wala kuogopa, nitaenda kufanyia kazi mapungufu ili mechi zijazo tufanye vizuri" amesema Baraza