Yanga yatangaza tarehe rasmi ya uchaguzi

Muktasari:

Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, alisema gharama za fomu hizo ni Sh 200, 000 kwa nafasi ya mwenyekiti na makamu wake huku kwa upande wa wajumbe ikiwa Sh 100,000.
Luigalangala alisema utaratibu wa kuchukua fomu malipo yake yanafanyika benki ili kupata akaunti namba ya malipo ni vyema wenye nia ya dhati ya kuiongoza Yanga  wakaenda kuchukua kwenye vituo tajwa.

BAADA ya  kuitikia wito wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), uongozi wa klabu ya Yanga umetangaza  kuwa uchaguzi mkuu  wa klabu hiyo utafanyika rasmi Januari 13 mwakani.
Uongozi wa Yanga jana ulikuwa na kikao na TFF kujadili masuala hanayohusu uchaguzi wao mkuu ambao utajikita kwenye kutafuta mwenyekiti, makamu wake pamoja na wajumbe.
Mara baada ya kikao hicho mbele ya waandishi wa habari leo hii,makao makuu ya TFF,  kaimu  mwenyekiti wa Yanga, Tobias Lungalangala ndiye aliyetangaza rasmi tarehe hiyo ya uchaguzi.
Mwenyekiti huyo aliyeambatana  na viongozi kadhaa wa TFF akiwemo kaimu mkurugenzi wa sheria wa shirikisho hilo, Rahimu Shaban, alisema zoezi la ugawaji fomu nalo  litaanza leo.
"Vituo ni viwili ambavyo vitatumika kwa wanaohitaji kuiongoza Yanga kujichukulia fomu, vituo hivyo cha kwanza ni hapa TFF na kingine ni makao makuu ya klabu yetu," alisema Luigalangala.
Hata hivyo kaimu huyo mwenyekiti wa Yanga, alisema gharama za fomu hizo ni Sh 200, 000 kwa nafasi ya mwenyekiti na makamu wake huku kwa upande wa wajumbe ikiwa Tsh 100,000.
Luigalangala alisema utaratibu wa kuchukua fomu malipo yake yanafanyika benki ili kupata akaunti namba ya malipo ni vyema wenye nia ya dhati ya kuiongoza Yanga  wakaenda kuchukua kwenye vituo tajwa.
Mwisho kaimu huyo mwenyekiti wa Yanga alimalizia kwa kusema hakutakuwa na kikao chochote kinachoihusu klabu hiyo hadi pale ambapo utafanyika uchaguzi mkuu Januari 13, mwakani.