Yanga yataka pointi za chee

Monday February 11 2019

 

By Charity James na Khatimu Naheka

SINGIDA United iliamsha sekeseke kwa kinda mmoja wa Yanga, Gustavo Simon, kijana mmoja fundi anayejua kutumia mguu wa kushoto wakidai sio halali kuichezea timu hiyo, lakini sasa Jangwani wakaamua kujibu mapigo wakizitaka pointi mbili za wapinzani wao.

Yanga na Singida zilitoshana nguvu kwa kutoka suluhu kwenye Uwanja wa Namfua na Singida kuibua zengwe kwa Gustavo, lakini nao wameamua kukimbili Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakitaka wapewe ushindi wa mchezo huo kwa vile wapinzani wao wamekiuka kanuni. Singida ilikata rufaa juu ya kinda huyo Gustavo wakisema hakutakiwa kuichezea Yanga kwani bado alikuwa na leseni ya klabu ya Dar City iliyopo Ligi Daraja la Kwanza.

Wakati shauri hilo likiwa bado halijapatiwa ufumbuzi ghafla nao Yanga nyuma yake wakafungua kesi kuishtaki Singida wakitaka nao wapokwe pointi kuwachezesha nyota wa wawili kimakosa. Yanga imewashtaki winga wao wa zamani Geofrey Mwashiuya na beki wao aliyewahi pia kukipiga Jangwani, Rajab Zahir wakidai wawili hao walifungiwa na kutozwa faini lakini hawakufanya hivyo.

Katika malalamiko yao Yanga imeitaka TFF kuipoka pointi Singida ikidai hawakutakiwa kumtumia Mwashiuya kutokana na winga huyo alifungiwa baada ya kubainika kumpiga mpinzani wake ngumi katika mchezo namba 195 kati ya Biashara dhidi ya Singida ambapo Mwashiuya alifungiwa mechi tatu na faini ya sh 500,000. Hali kadhalika Zahir aliyepewa kadi nyekundu kama Mwashiuya kwenye mchezo huo, japo yake ilikuwa ni baada ya mchezo kumalizika kufuatia kufanya kosa la kutaka kumpiga mwamuzi ambapo alifungiwa adhabu kama hizo za Mwashiuya.

Madai ya Yanga yako hivi licha ya wachezaji hao kumaliza adhabu ya kutumikia mechi hizo lakini hawakuwa wamelipiwa faini walizotakiwa kulipa jumla ya sh 1,000,000 na kucheza mechi dhidi ya Yanga.

Malalamiko yote yapo TFF yakisubiri maamuzi ya kujua klabu ipi iko sahihi katika madai yao ambapo timu zote mbili zimetaka kupewa pointi tatu katika mechi baina ya timu hizo. Uongozi wa Yanga ulitafutwa kutoa ufafanuzi wa rufaa yao, hiyo lakini walikuwa bize na mechi yao ya jioni dhidi ya JKT Tanzania.

Advertisement