Yanga yashtuka, yajipa taji la 28

Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera

Muktasari:

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Omari Kaya amesema baada ya matokeo ya Simba wamepata akili kwamba timu yao inaweza kupigania ubingwa.
Kaya amesema mpaka sasa Yanga imepata matokeo mazuri katika mechi zaio tatu ngumu ambazo msimu uliopita ziliwasumbua.
Amesema endapo watafanikiwa kuitunza timu yao kama walivyopanga suala la kupata ubingwa litakuwa ndani ya uwezo wao.

KIKOSI cha Yanga kikiwa bila Kocha Mkuu wake, Mwinyi Zahera usiku wa leo kitashuka kwenye Uwanja wa Taifa, kuvaana na Mbao FC, huku mabosi wake wakishtuka na kuanza kujipa mapema taji la ubingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

Yanga ndiyo inayoshikilia rekodi ya kubeba mataji mengi ya Ligi Kuu tangu mwaka 1965 ikinyakua mara 27, lakini matokeo mazuri ya mechi zao tano za awali walizocheza hasa dhidi ya Simba limewafanya mabosi kuamini wanabeba tena msimu huu kufikisha la 28.

Msimu uliopita, timu hiyo ilipoteza taji walilokuwa wakilishikilia kwa misimu mitatu mfululizo baada ya kuzidiwa na watani zao, Simba hasa baada ya Yanga kuwa na kikosi dhaifu na huku wakisumbuliwa na suala la kiuchumi, lakini viongozi wa klabu wanaona kuna kitu tofauti wanaweza kukifanya kurudisha mataji hilo tena.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Omari Kaya amesema mpaka sasa tathimini yao kama viongozi wanaona kikosi cha kupata mataji msimu huu kipo kamili kwa aina ya matokeo waliyopata na jinsi wachezaji wanavyojituma uwanjani.

Kaya alisema Yanga ya msimu huu imethibitisha hilo kuwa ipo gado baada ya kupata matokeo mazuri katika mechi tatu ngumu walizotumia kama kigezo cha kujitathmini.

Alisema kitendo cha Yanga kuifunga Mtibwa Sugar kisha kufanya hivyo dhidi ya Singida United huku wakipata pointi moja katika mechi ya Simba ni matokeo yanayoonyesha utofauti mkubwa wa kikosi chao cha sasa na kile cha msimu uliopita.

“Uongozi tunaona kikosi cha ubingwa tunacho hatuna wasiwasi mpaka sasa, ukiangalia kuna mechi zilizotusumbua katika hesabu zetu msimu uliopita safari hii zote tumepata matokeo mazuri,” alisema Kaya na kuongeza.

“Tumewafunga Mtibwa na Singida ambao walitusumbua msimu uliopita, lakini pia tukapata pointi moja na Simba ukiangalia mechi hizi ina maana hapo tumebakiza ni Azam pekee ndio tishio lakini mpaka sasa tumepata matokeo ambayo yanatupa ujasiri kwamba msimu huu tuna timu bora ya ushindani.

Aidha, Kaya alisema wanachofanya sasa kama uongozi ni kujipanga sawasawa katika kuihudumia timu hiyo kuhakikisha maslahi ya wachezaji yanakuwa sawa na endapo hilo litafanikiwa ubingwa hautakwepeka kutua kwao.

“Wanachama wetu wanatakiwa kuiunga mkono timu yetu kokote tunakokwenda na hata wakiweza kuichangia waichangie kwa wingi,huku uongozi tumejipanga sawasawa kuhakikisha tunaelekeza nguvu kubwa katika kuihudumia timu.

“Tukifanikiwa kuweza kumudu gharama za kuilea timu kwa kuitunza sawasawa hatutakuwa na sababu ya kutopata ubingwa msimu kwa jinsi ambavyo timu yetu tulivyoiona.”

KAZI IPO TAIFA

Yanga leo usiku itaikaribisha Mbao FC ambayo tangu ipande msimu wa 2016-2017 haijawahi kupata ushindi kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya wapinzani wao hao, ingawa inapochezwa CCM Kirumba haijawahi kupoteza kwa Yanga katika michuano yoyote kwamba kila mmoja mbabe kwake.

Mbao iliifunga Yanga katika mechi ya robo fainali ya Kombe la FA misimu miwili iliyopita kabla ya kutibua sherehe za ubingwa kwa klabu hiyo kwa kuwachapa siku chache baadaye msimu wao wa kwanza wa Ligi Kuu.

Msimu uliopita walirudia tena kuwatia adabu Yanga kwa kuwacharaza mabao 2-0 pale Kirumba, ingawa mechi zote za ugenini jijini Dar kwa misimu hiyo miwili ilipoteza kwa mabao 3-0 na 1-0.

Hata hivyo, msimu huu Mbao imeonekana imekuja kivingine kwani kabla ya mechi za jana ilikuwa nafasi ya pili ikiwa na alama 15, moja pungufu ya walizonazo vinara Mtibwa Sugar na iliandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuizima Simba kwa kuilaza bao 1-0 CCM Kirumba.