Yanga yapanda nafasi ya pili kibabe, Yikpe atupia

Muktasari:

 Yikpe ni goli lake la pili kwa Yikpe msimu huu katika Ligi Kuu.

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Yikpe Gnamien ameinua mashabiki wa Yanga kwa shangwe baada ya kuifungia timu hiyo goli la tatu katika mchezo wao dhidi ya Singida.

Shangwe hizo ziliibuka kutokana na mchezaji huyo kuwa na kosa kosa nyingi katika michezo ya awali, hivyo baada ya kufunga alifanya mashabiki washangilie wengine wakiishia kucheka jukwaani.

Baada ya kufunga goli hilo, Yikpe alienda kushangilia kwa staili ya kukaa chini huku shangwe zikitawala uwanjani.

Ushindi huo unawafanya Yanga kufikisha pointi 67 na kusogea mpaka nafasi ya pili na kuwashusha Azam wakiwa na pointi 65.

Katika kipindi cha kwanza Yanga walionyesha kuhitaji goli la kuongoza lakini mahesabu yao yalikuwa hayaki vizuri.

Dakika 33 Yanga ilipata bao la kuongoza kupitia kwa Paul Godfrey baada ya winga Mrisho Ngassa kukimbia na mpira kisha ilitokea piga nikupige langoni mwa Singida na Godfrey alitupia wavuni.

Dakika 36 Yanga ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Rafael Daud na kuingia Ditram Nchimbi.

Dakika 37 Yanga ilipata bao kupitia kwa Mrisho Ngassa akiitumia vizuri pasi ya Deus Kaseke, Ngassa aliuruka mpira ndani ya boksi na kumuangalia kipa wa Singida United, Owen Chaima na kupiga mpira ulioenda moja kwa moja wavuni.

Dakika 42 beki wa Singida, Reward Mshanga alionyeshewa kadi ya njano baada kumfanyia madhambi Paul Godfrey

Dakika 45+ Singida walipata goli la kwanza kupitia kwa Stephen kupitia kona ya Rowadr Mshanga na Stephen alionganisha kwa kichwa.

Kiungo wa Singida, David Nartey alionyeshewa kadi ya njano dakika 50 baada ya kumzuia winga wa Yanga, Patrick Sibomana alipokuwa anajaribu kumtoka wakati huo dakika 54 mshambuliaji wa Singida Utd, Stephen Sey alionyeshewa kadi ya njano baada ya kumkanyaga Lamine Moro.

Yanga ilifanya mabadiliko dakika 60 kwa kumtoa David Molinga na Patrick Sibomana na kuingia Ally Mtoni na Yikpe Gislain.

Mabadiliko hayo yalimfanya Yondani akacheze kwenye eneo la kiungo sambamba ma Makame, huku Mtoni akicheza na Lamine kwenye eneo la beki.

Dakika 62 Yanga ilitaka kupata bao kupitia kwa Mrisho Ngassa baada ya kufyatuka shuti kali nje ya boksi akipokea pasi ya Ditram Nchimbi lakini shuti hilo lilidakwa vizuri na kipa Owen Chaima.

Dakika 69 Yikpe aliwainua mashabiki kwa shangwe uwanja mzima baada ya kuifungia Yanga goli la tatu akipokea pasi ya Abdulaziz Makame na yeye kutulia kisha akamtoka kipa Owen Chaima na kutupia wavuni.

 

Dakika 73 Yanga ilitaka kupata bao la nne lakini umakini wa mshambuliaji Yikpe Gnamien ulikuwa hafifu na kujikuta wakikosa goli hilo.

Yanga ilifanya mabadiliko mengine dakika 76 kwa kuwatoa Mrisho Ngassa na kuingia Eric Kabamba.

Dakika 81 mshambuliaji wa Singida Utd, Emmanuel Manyanda alitaka kuifungia bao la pili baada ya kuwapangua mabeki wa Yanga, Paul Godfrey na Lamine Moro kisha alifyatuka shuti kali lakini kipa Faruk Shikhalo alilipangua kisha na kulidaka kwa umakini.

Singida walifanya mabadiliko ya kuwatoa, Stephen Opoku na Seiri Arugumayo na kuingia Ramadhan Hashimu na Aldof Anthony.