Yanga yanasa visu matata

Eliud  Ambokile

Muktasari:

  • Kuvunjwa kwa mkataba wa Bigirimana kumbe Yanga wanahusika ni baada ya kufunguka kuwa amefuatwa na viongozi wa timu hiyo, SPOTANZA klabu haina mamlaka ya kumfungia mchezaji.

YANGA ipo Shinyanga na jioni ya leo Alhamisi inavaana na Mwadui katika mechi ya kiporo cha Ligi Kuu Bara, huku ikiwakosa nyota wake, lakini kama kuna jambo linafanya na mabosi wao na huenda litawapa furaha mashabiki wa klabu hiyo.

Katika kuhakikisha Yanga inaondokana na tatizo la safu ya ushambuliaji, mabosi wa timu hiyo inaelezwa wameanza mchakato wa kuwanasa mastraika wawili

matata ili kuwasaidia kina Heritier Makambo na Ibrahim Ajibu ‘Kadabra’.

Ipo hivi. Dirisha la usajili la Ligi Kuu Bara lilifunguliwa Novemba 15 na litafungwa katikati ya mwezi ujao, lakini Yanga wamekuwa wakifanya mambo yao kimya kimya ikielezwa imeshazungumza na kinara wa mabao, Eliud Ambokile wa Mbeya City na Mrundi Bigirimana Blaise wa Stand, huku Sixtus Sabilo pia wa Stand akitajwa kuwa katika rada za mabosi hao wa Jangwani.

Hata hivyo inaelezwa kuwa uamuzi wa straika gani watue Yanga ipo mikononi mwa Kocha Mwinyi Zahera ambaye amekiri anapata ugumu wa kufanya uamuzi kwa sasa kutokana na hali ngumu iliyopo klabuni kwao. Habari za ndani zinasema kuwa viongozi wa Yanga wamekuwa wakiwafukuzia wachezaji hao na kuzungumza nao ili kutekeleza ombi la kocha wao kutaka atafutiwe straika matata na winga moja wa kuifanya timu iwe na uhai zaidi ya kuzalisha mabao kulijko ilivyo sasa.

Inaelezwa hata kufungiwa kwa kina Sabilo na Bigirimana kulikofanywa na mabosi wao wa Stand ni kutokana na kusikia tetesi za kutakiwa na Yanga, japo viongozi wa Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA) wamekiri klabu haina uwezo wa kumfungia mchezo zaidi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

MRUNDI HUYU HAPA

Bigirimana aliyepo kwao Burundi kwa sasa, amekiri kutafutwa na Yanga ili ajiunge nayo, huku akifichua kuwa pia kuna ofa nyingine tatu kutoka Alliance, Ndanda na KMC zinazomhitaji.

Bigirimana alisema bado hajaamua atatua wapi kutokana na kuwa yupo katika hatua ya kuvunja mkataba na Stand United ambao alisema hawajamtimizia baadhi nya madai yake ikiwemo fedha za usajili.

“Malengo yangu ni kucheza timu kubwa ndio maana naendelea na mazungumzo na viongozi wangu, kwani hata ile adhabu waliyonipa ya kukaa miezi sita ilifutwa ili kama ikiwezekana tuachane vizuri,” alisema Bigirimana.

Naye Ambokile alisema ni kweli Yanga wamemtafuta kwa njia ya simu wakihitaji huduma yake lakini kikubwa alicho wajibu ni kuwataka waonane na uongozi wa timu yake ya Mbeya City kutokana na kuwa na mkataba nao.

MSIKIE NYIKA

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu ya Yanga, Hussein Nyika kutolea ufafanuzi juu ya wachezaji hao alisema muda wa wao kuzungumzia suala la usajili

ukifika watafanya hivyo.

“Bado hatujaanza kusajili na tukianza kila mmoja atalifahamu hilo kuhusu wachezaji kufuatwa na kuzungumza nao juu ya usajili kipindi hiki ni kawaida lakini wishu ikikamilika ndio tunaweza kuwa la cha kuongea,” alisema.

ZAHERA HANA PRESHA

Katika hatua nyingi Kocha Zahera alisema licha ya kuwakosa nyota wake katika mchezo wao wa leo mjini Shinyanga baada ya kugoma kama shinikizo la kutaka

malipo yao ya mishahara ya miezi karibu mitano bado hana presha yoyote.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Mwanza alipotua akitoka kwao DR Congo, Kocha Zahera alisema kukosekana kwa Kelvin Yondani na Beno Kakolanya haimpi

presha katika mchezo wao wa leo na matarajio yao ni ushindi.

“Haitupi presha, Yanga ni kubwa na ina kikosi kipana, hao wasipokuwepo ina maana nawapanga wengine, tumejipanga nje na ndani ya Uwanja wa Taifa, lazima tushinde mechi ya kesho (leo),” alisema Zahera.