Yanga yamtesa Kitenge

Muktasari:

Kitenge; Hata kuwafunga Yanga nilikutana na vikwazo hivyo bado nitaendelea kupambana ili kuondoa gundu inayoniandama kwasasa kwani tangu nifunge katika mchezo wetu na Yanga sijapata nafasi ya kufunga tena.

MSHAMBULIAJI wa Stand United, Alex Kitenge amesema mzimu wa kuifunga Yanga bado unamtesa baada ya kukutana na ugumu kutoka kwa mabeki wa timu pinzani hasa wanapokutana kwenye mechi.

Kitenge hadi sasa hajafunga bao lolote tangu awafunge Yanga mabao matatu ‘hat-trick’ katika mchezo wa ligi na Yanga ilishinda mabao 4-3. Mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kitenge alisema amekuwa akikutana na changamoto ya kukamiwa na mabeki kitu ambacho kimekuwa kikimuwia vigumu kufunguka na kuisaidia timu yake kwa kuifungia mabao.

“Sijakata tamaa ninapambana na naamini nitaondoa gundu hiyo nawahakikishia viongozi na mashabiki wangu kuwa bado nina nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika michezo iliyobaki kwani, napambana kutafuta mbinu ya kuwatoka mabeki wanao ninyima nafasi ya kufunga.

“Mwalimu wangu ana imani na mimi na ndio maana amekuwa akinipanga kila mchezo pamoja na kukosa nafasi ya kufunga anaamini siku nitaweza kufanya hivyo na nikawashangaza wengi, sipo tayari kumuangusha naamini nitaweza kufanya hivyo,” alisema Kitenge.

Aliongeza kwa kukanusha baadhi ya maneno yanayozungumzwa kuwa alibahatisha kuwafunga Yanga na kuweka wazi kuwa alikutana na changamoto kubwa pia kuwafunga na kuweka wazi haikuwa kazi rahisi kama wanavyomzungumzia.